Kombe la Waitara Golf kutimua vumbi Machi 22

SHINDANO la mchezo wa Gofu kumuenzi Mkuu wa Majeshi wa zamani Jenerali mstaafu George Waitara linatarajia kufanyika Machi 22 kwenye viwanja vya Gofu Lugalo, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali mstaafu Michael Luwongo amesema leo kuwa wanatarajia ushiriki mkubwa wa wachezaji kutoka klabu mbalimbali nchini.

Amesema anaamini shindano hilo litakuwa lenye ushindani mkubwa kwa kuwa litashirikisha wachezaji wakubwa na wenye uzoefu katika michuano mikubwa.

Waitara ni muasisi wa klabu ya Lugalo na ndiye muanzilishi wa viwanja vya Gofu kwenye klabu hiyo hivyo wanamuenzi kutambua mchango wake katika michezo nchini.

“Nawashukuru benki ya NBC ambao kila mwaka wanadhamini shindano hili. Mwitikio wa washiriki ni mkubwa na tunategemea watakuwa wengi sana. Washiriki ni wa madaraja yote kuanzia watoto, vijana, wanawake na wazee,”amesema.

Amesema washindi wote watapewa zawadi mbalimbali zilizoandaliwa kwa kila daraja katika hafla itakayofanyika siku hiyo jioni.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko Benki ya NBC, David Raymond amesema wao kama wadau wakubwa wa michezo wana dhamira ya dhati ya kukuza mchezo huo.

Amesema huu ni msimu wa nne wamekuwa wakidhamini shindano hilo na kutoa wito kwa washiriki kujitokeza kwa wingi kuona shindano hilo.

Nahodha wa Gofu Lugalo Meja Japhet Masai amesema droo ya shindano hilo kwa ajili ya kupanga timu na wachezaji itafanyika kesho.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button