Rifaly, Stanbic wawapiga jeki waunda maudhui

DAR ES SALAAM: Rifaly, kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania, leo wameandaa tukio la pili la ‘Creators Day’, likiwa na kaulimbiu ya “Kugeuza Ubunifu Kuwa Fursa: Mustakabali wa Kutengeneza Kipato Kupitia Maudhui ya Kidijitali.” Tukio hili limefanyika katika Ukumbi wa Stanbic Biashara Incubator jijini Dar es Salaam na kukutanisha waundaji maarufu wa maudhui, viongozi wa biashara, wataalamu wa fedha, pamoja na mamlaka za udhibiti nchini.
Lengo kuu la tukio hili ni kuwakutanisha na kuwawezesha waundaji wa maudhui nchini Tanzania kwa kuwapa mikakati ya vitendo na nyenzo muhimu za kutengeneza kipato kupitia maudhui yao. Kadiri sekta ya maudhui nchini Tanzania inavyokuwa, waundaji wa maudhui wanahitaji zaidi elimu ya fedha, mitandao imara ya kibiashara, pamoja na mazingira bora ya kisera ili kujenga biashara endelevu kutokana na ubunifu wao.
Ukuaji wa sekta hii ya ubunifu unafungua fursa mpya kwa sekta mbalimbali nchini Tanzania. Taasisi za fedha zinaweza kutoa huduma mahsusi za kibenki kwa wajasiriamali wa kidijitali. Makampuni na watangazaji yanaweza kupata urahisi wa kufikia hadhira kubwa kupitia ushirikiano na waundaji wa maudhui. Vyombo vya habari navyo vinanufaika kutokana na maudhui mbalimbali yenye mvuto kutoka kwa wazalishaji wa ndani, huku mamlaka za udhibiti zikisaidia kujenga mazingira yanayowawezesha waundaji kukua kwa uwajibikaji.
Akitoa neno la ufunguzi, Kai Mollel, Mkuu wa Kitengo cha Biashara Incubator kutoka Stanbic Bank Tanzania, alisisitiza dhamira ya benki hiyo katika kusaidia ukuaji wa Biashara Ndogo na za Kati (SME), ikiwemo wajasiriamali wa kidijitali na waundaji wa maudhui.
“Tunatambua kuwa waundaji wa maudhui wana nafasi kubwa katika uchumi, hivyo Stanbic tumejipanga kikamilifu kuhakikisha wanajenga misingi sahihi ya kibiashara ili kufanikiwa,” alisema Kai.
Katika hotuba ya utangulizi, Loth Makuza, Kiongozi Mwandamizi wa Rifaly, alifafanua zaidi dhana ya Uchumi wa Ubunifu (Creatos Economy), akionyesha fursa zinazoibuka za kutengeneza kipato kupitia maudhui ya kidijitali Tanzania.
“Sekta ya ubunifu wa maudhui nchini Tanzania inakua kwa kasi kubwa. Lengo letu ni kuwawezesha waundaji wa maudhui kupitia nyenzo mbalimbali, fursa za kifedha na kuwakutanisha moja kwa moja na makampuni na watangazaji,” alisema Loth.
Baada ya hotuba ya ufunguzi, Mika Chavala, mwanzilishi wa Swahili Nation na mwanamitandao maarufu, aliwasilisha mada kuhusu “Kuelewa Namna ya Kutengeneza Kipato Kupitia Maudhui.” Mika alielezea mambo muhimu kama uthabiti (consistency), kujijengea jina (branding) na kujiweka kimkakati katika soko.
“Waundaji wa maudhui lazima wajitofautishe na waondoke katika maeneo yao ya kawaida ili kupata mafanikio zaidi,” alisema Mika.
Kipindi cha majadiliano kilichoongozwa na Subira Bawji, mwanzilishi wa Enderera Investment, kilifuatia. Wachangiaji wakuu katika majadiliano hayo walikuwa Sharon Mujuni, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Biashara na SMEs, Stanbic Bank Tanzania; Mika Chavala; Kelvin Kimbeje, mtaalamu wa elimu ya fedha na uundaji wa maudhui; pamoja na Brian Kalinga kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Miongoni mwa hoja muhimu zilizotolewa ni:
Sharon Mujuni alielezea kuwa Stanbic Bank imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na SME za Tanzania, wakiwemo waundaji wa maudhui, ili kuwajengea misingi thabiti ya biashara.
Kelvin Kimbeje alisisitiza umuhimu wa elimu ya fedha kwa waundaji wa maudhui. “Ni muhimu kwa waundaji kujua namna ya kutafuta pesa, kuzitunza, kuzihifadhi na kuwekeza,” alishauri Kelvin, akihimiza pia umuhimu wa kuwa na vyanzo mbalimbali vya mapato.
Brian Kalinga alisisitiza umuhimu wa maudhui yenye maadili na yenye hadhi katika jamii.
Alifafanua kuwa TCRA inashirikiana na serikali kuweka mazingira bora ya kisheria na kisera ili kuendeleza maudhui ya ndani. Mojawapo ya mikakati iliyopo ni kuhakikisha vituo vya redio na televisheni nchini Tanzania vinarusha zaidi maudhui ya ndani.
Mwisho wa tukio, Loth Makuza alisisitiza tena dhamira ya Rifaly katika kusaidia waundaji kupitia jukwaa lao la kidijitali.
“Hapa Rifaly, Watengenezaji wa maudhui wanalipwa dola 10 kwa kila maudhui 10 wanayopakia kwenye jukwaa letu,” alisema Loth, akieleza jinsi Rifaly inavyowaunga mkono watengenezaji wa maudhui kidijitali.
Siku ya watengeneza maudhui imeshuhudia ushiriki mkubwa kutoka kwa waundaji wa maudhui waliofika kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania, huku wakishiriki kikamilifu kwenye majadiliano. Kutokana na mafanikio haya, Rifaly imejipanga kuandaa matukio zaidi kama hili ili kuwezesha zaidi sekta ya ubunifu Tanzania



