IRINGA: Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakipo tayari kwenda kinyume na katiba na sheria kwa sababu hakitaki kupitisha muda uliowekwa wa Rais, wabunge na madiwani kukaa madarakani, hivyo watashiriki uchaguzi pamoja na vyama vingine vya upinzani ambavyo vipo tayari kushiriki uchaguzi mkuu.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla aliyasema hayo leo Machi 29,2025 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa Iringa Mjini mkoani Iringa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku tatu mfululizo katika mikoa miwili ya Mbeya na Iringa.
Aidha, Makalla amesema kuwa uchaguzi mkuu upo kwa mujibu wa katiba na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio kwa matakwa ya CCM, hivyo kutokushiriki ni kwenda kinyume na katiba ambayo iliyopo sasa na CCM kama chama tawala wamesema hawapo tayari kwenda kinyume na muongozo huo wa katiba unavyoelekeza.
“Sisi tutaendelea na uchaguzi uchaguzi huu upo sio kwa matakwa ya CCM uchaguzi huu upo kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katiba tuliyonayo leo wanataka kuikanyaga je wataweza kuitekeleza katiba mpya,” amesema Makalla.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa katiba inaelezwa kuwa Rais, madiwani na wabunge waliopo madaraka wanatakiwa wachaguliwa kila baada ya miaka mitano, alisistiza kuwa CCM ni chama kinachojali demokrasia hawataki kuzidisha miaka mitano bila kufanya uchaguzi ili kufuata katiba inavyoeleza.
Makalla amesema wapo tayari kushiriki uchaguzi pamoja na vyama vingine vya siasa vilivyopo tayari kushiriki uchaguzi ili kufuata takwa la katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sambamba na hayo Makalla ameeleza sababu zilizopelekea Chadema kutokutaka kushiriki uchaguzi moja ya sababu akidai kuwa ni kutokujiandaa kwa chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu na kuongeza kuwa migogoro iliyopo ndani ya chama hicho imeleta mpasuko na kupelekea kutokuwa tayari kwa kutofautiana kwa hoja baina yao.
Makalla amesema kuwa pamoja na Chadema kutokuwa tayari kushiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwaka huu wapo wanachaka waliopo ndani na wanashauku ya kugombea nafasi mbalimbali zikiwemo madiwani na wabunge, hivyo amewataka wasikate tamaa na kwenda kugombea katika vyama vingine ili kutimiza ndoto zao.