Muuguzi asimamishwa tuhuma za kubadilisha mtoto

WIZARA ya Afya imemsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia mkazi wa Daraja Mbili mkoani Arusha baada ya kuripoti kubadilishiwa mtoto aliyejifungua kwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru mkoani humo.

Pia, imechukua sampuli za wazazi waliojifungua kipindi hicho pamoja na za watoto kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba.

Taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya, Roida Andusamile jana ilieleza Neema Kilugala alijifungua Machi 24, mwaka huu kwa njia ya upasuaji na muuguzi huyo alimwonesha mtoto wake akiwa mzima na baadaye aligundua amebadilishiwa mtoto.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa mujibu wa mama wa mtoto (Neema), baada ya kuletewa mtoto, alibaini vitenge alivyokuwa amefungwa navyo si vyake.

“Muuguzi wa hospitali hiyo alidai kuwa alichanganya vitenge na vya mtoto mwingine hivyo akaahidi kwenda kubadilisha, pamoja na kuchukua hatua hiyo bado kulikuwa na hali ya sintofahamu,” ilieleza taarifa ya Andusamile.

Alieleza kwamba kutokana na hali hiyo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha pamoja na Jeshi la Polisi imechukua hatua ya kuchukua sampuli za wazazi waliojifungua kipindi hicho pamoja na za watoto kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Pia, hatua nyingine iliyochukuliwa ni kumsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia ili kupisha uchunguzi na kwamba baada ya uchunguzi kukamilika, taarifa rasmi zitatolewa na hatua stahiki zitachukuliwa.

Akizungumza na mtandao wa Millard Ayo, mama wa mtoto huyo, Neema alidai baada ya kufanyiwa upasuaji aliambiwa kwamba mtoto wake yupo kawaida akiwa na kilogramu 3.1 na walimuuliza kama ana ndugu, aliwaambia yupo mama yake.

“Walinifuata na kunipeleka kwenye chumba cha kupumzika na saa saba kasoro nililetewa mtoto ambaye alifungwa vitenge si vyangu, nilimtaarifu mama akamuita nesi na kumwambia aturudishie mtoto. Alirudi bila mtoto na kuanza kunizungusha huku wakiniambia mtoto yupo kwenye chumba cha joto,” alidai Neema.

Alihoji sababu za mtoto wake kupelekwa kwenye chumba cha joto wakati alipojifungua hakuambiwa kama ana tatizo lolote la kiafya.

“Waliniambia mtoto yupo vizuri, lakini amehifadhiwa katika chumba cha joto, walinizungusha nikasubiri asubuhi nilipokwenda kumuona yule si mtoto wangu, sijui walimpeleka wapi mtoto wangu, nisingefanyiwa upasuaji asingepotea. Namtaka mtoto wangu alikuwa mweupe,” alisisitiza Neema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button