Saba wapandikizwa nyonga, magoti Mloganzila

DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji wa upandikizaji wa marejeo wa nyonga na magoti kwa wagonjwa saba katika kambi maalumu ya siku nne kuanzia Aprili 14 hadi 17,2025.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk Godlove Mfuko amesema tangu kuanza kwa upasuaji wa magoti na nyonga bandia mwaka 2022 zaidi ya wagonjwa 275 walipata huduma hiyo.
Aidha amesema katika kliniki ya mifupa ,ugonjwa wa nyonga na magoti unashika nafasi ya pili baada ya matatizo ya mgongo ambapo kuanzia Januari hadi Machi 2025 waliwaona wagonjwa 4,513 kati yao 1,527 walikuwa na matatizo ya nyonga na magoti.
“Hii ni sawa na asilimia 34 ya wagonjwa wote,kwa wastani kwa mwezi tunaona wagonjwa 450 hadi 550 wenye matatizo hayo na tumeshirikiana hospitali mbalimbali nchini kama Temeke, CCBRT.”
Dk Mfumo ameeleza kuwa awali upasuaji huu ulikuwa haufanyiki kwasababu ya ujuzi na vifaa vya upandikizaji wa marejeo vilikuwa havipo hivyo sasa upasuaji huo utakuwa endelevu.
“Matibabu haya ni mkakati wa serikali ya Rais Samia huduma bobezi kuwafikia wananchi waliko na tumefanya upasuaji huu kwa kushirikiana na wataalamu kutoka China.
Amebainisha kuwa gharama za matibabu kwa mtu mmoja nje ya nchini ni kiasi cha Sh milioni 27 ambapo ndani ya nchi ni Sh milioni 13.5.
“Kwa bahati mpaya hakuna bima katika matibabu haya tutakaana na wenzetu wa bima ili tujadili namna ya kuingiza hili katika bima.
Kwa upande wake Daktari Bingwa Bobezi wa Nyonga na Magoti,Shilekirwa Makira amesema sababu za kusagika kwa mifupa hiyi ni ya kimaumbile.
“Kuna mtu kadiri umri unavyosogea anaweza kupata changamoto,nyingine ni maradhi kama pumu ya mifupa ambayo mtu anakuwa nayo tangu akiwa mdogo,nyingine ni ajali kama ukipata ukiwa na umri mdogo na mfupa haujarudishwa vizuri unaweza kupata.
Amesema ugonjwa huo unawakumba zaidi watu wenye umri kuanzia miaka 60 kwenda juu na wenye ugonjwa wa selimundu.
“Ukifanyiwa mara ya kwanza unakaa miaka 20 hadi 25 ikitokea changamoto unalazimika kufanya upasuaji wa marejeo na wengine wakipata maambukizi au ajali hao tunawafanyia upasuaji wa marejeo.
Amewashauri watu kufuatilia kwa madaktari mapema ili kupewa virutubisho vinavyocheleweza kusagika kwa magoti na nyonga na waliofanyiwa upasuaji wazingatia matibabu yote ili wasipate maambukizi.
Mmmoja wa madaktari wa Hospitali ya Macho CCBRT walioshiriki upasuaji huo Dk Prosper Alute amewashukuru Mloganzila kwani upasuaji wa awali unafanyika kwa kiasi kikubwa lakini wa marejeo unafanyika kwa uchache.
“Tunaamini tutaendelea kujifunza kutoka kwa madaktri wengine na tutafanya huduma hizi katika vituo vyetu.



