Mahakama Kuu yaipa Chadema siku 21

DAR ES SALAAM – MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetoa siku 21 kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwasilisha mahakamani utetezi wa maandishi katika kesi inayokikabili.

Jaji Hamidu Mwanga alitoa amri hiyo mahakamani hapo jana wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye anajitambulisha kama mwanachama na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao wanajitambulisha kuwa ni wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho ni mdaiwa wa pili. Chadema inawakilishwa na mawakili, Jeston Justine na John Chogomo wakati upande wa walalamikaji unawakilishwa na wakili, Shaban Marijani.

Wakili Justine akisaidiana na Chongomo waliiomba mahakama iwape muda usiopungua siku 21 kuandaa na kuwasilisha utetezi wake kwa mujibu wa sheria.

Wakili wa walalamikaji, Miraji hakuwa na pingamizi dhidi ya ombi hilo na Jaji Mwanga aliliridhia. “Maombi ya upande wa wadaiwa yamekubaliwa na wanapewa siku 21 kutoka leo Aprili, 17, 2025 kuwasilisha utetezi wake.

Hivyo, wadaiwa mnaelekezwa kuwasilisha mahakamani utetezi wenu kufikia au kabla ya Mei 21, 2025,” alisema Jaji Mwanga.

Aidha, Jaji Mwanga alipanga kesi hiyo kutajwa tena mahakamani hapo Mei 12, 2025 ili kuona kama maelekezo aliyoyatoa yamefanyiwa kazi na kama yatakuwa yamekamilika ili amri nyingine muhimu ziweze kutolewa.

PIA SOMA: Timu ya MSLAC yamsadia mtoto Loveness kuanza shule

Katika kesi hiyo wadai wanaiomba mahakama itoe tamko na kuamuru wadaiwa kuonesha wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa pamoja na katiba ya chama hicho.

Waliendelea kueleza wameomba mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama pamoja na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Wanadai kuna ubaguzi wa kidini, kijinsia na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano. Walalamikaji wanaomba mahakama itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kuwa wamekiuka kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 marejeo ya mwaka 2019.

Aidha, wanaiomba mahakama itamke kuwa ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile wanaiomba mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia Kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 marejeo ya mwaka 2019.

Pia, wanaomba kusitishwa kwa muda shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwa na utekelezaji wa maagizo ya mahakama na itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.

Wadai pia, wanaiomba mahakama iamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo mahakama hiyo itaona inafaa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button