Kimei ahoji mpango wa serikali kukarabati masoko ya vijijini
DODOMA;
MBUNGE wa Vunjo, Dk Charles Kimei (CCM) amehoji serikali akitaka kujua ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya masoko ya vijijini nchini, ikiwemo sakafu na paa.
Serikali ikijibu imesema, imejenga na kukarabati masoko 264 kati ya 1,056 yaliyopo katika halmashauri za wilaya kote nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Festo Dugange alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Sh bilioni 12.2 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa masoko ya vijijini.
“Tayari kiasi cha Shilingi bilioni 1.5 zimeshatolewa,” alisema Dugange.
Aliongeza: “Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya masoko ya vijijini kwa kujenga na kukarabati paa na sakafu ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kuuza bidhaa zao katika mazingira salama”.
Katika swali la nyongeza, Dk Kimei alitaka kufahamu kauli ya serikali itafanya nini kutokana na masoko makongwe kama ya Chekereni, Himo, Mwika ambayo ni kitovu cha ajira kwa vijana na masoko hayo hayana miundombinu na kuomba fedha zikitolewa masoko hayo yaboreshwe.
“Mji wa Himo kihistoria umekuwa wa kimataifa kwa soko la nafaka ambapo nchi jirani wakija Himo na baadaye soko lilikufa na kuna eneo la Lokolova lina ekari 140, lini litajengwa soko hapo,” alihoji.
Dugange akijibu maswali hayo alisema mwaka uliopita kulitengwa Sh milioni 20 na mwaka huu Sh milioni 20 tena kwa ajili ya kuboresha masoko hayo na tayari fedha hizo zishapelekwa kwenye halmashauri husika.
Alisema Halmashauri ya Moshi inatafuta hati kwenye eneo la Lokolova na ikipatikana itaanza ujenzi kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Naye Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave (CCM) alitaka kufahamu serikali ina mpango gani kutengeneza Soko la Keko ikizingatiwa linatengeneza samani.
Dugange alisema: “Ni wajibu wa Manispaa ya Temeke kuweka kipaumbele cha maboresho ya soko hilo na kutenga bajeti”.



