TRA yasisitiza matumizi sahihi huduma mitandaoni

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita imewaomba wafanyabiashara na wananchi wote kutumia kwa ufasaha huduma za TRA zinazotolewa mtandaoni ili waweze kupata huduma kwa wakati.
Ofisa Elimu kwa Mlipakodi TRA mkoa wa Geita, Justine Katiti amesema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari wakati wa kilele cha maonyesho ya wakandarasi yaliyofanyika mjini Geita.
Amesema kwa sasa huduma nyingi za TRA zinatolewa kwa njia ya mtandao ikiwemo usajili wa walipa kodi na kutoa Namba ya Mlipakodi (TIN) ili kusaidia wananchi kupata huduma kwa wakati.
“Sasa hivi TRA huduma nyingi tunatoa kwa njia ya mtandao ili kuweza na kurahisisha ulipaji wa kodi, na watu kutopoteza muda sana kwa kuwa na ulazima wa kwenda ofisi za TRA”, amesema Katiti. 
Amesema TRA imejidhatiti kutoa elimu kwa wananchi kuweza kujisajili na waweze kupata huduma kwa njia ya mtandao ikiwemo kupata TIN, Control Number kutuma taarifa za mlipa kodi (returns).
“Mpaka sasa kuna maboresho mengine zaidi katika mfumo ikiwemo usajili wa magari, pamoja na leseni za udereva, hizi zote sasa hivi zinapatikana kwa njia ya mtandao”, amesisitiza Katiti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Bernard Kavishe amesema ili kukuza mnyororo wa thamani ya ulipaji kodi ni lazima sheria ya uwezeshaji wazawa iwekewe mkazo.
Amesema iwapo kampuni za ndani zitapewa nguvu kupitia sheria ya uwezeshaji wazawa (local contents acts) kwenye sekta mbalimbali ikiwemo itapanua uwigo wa ajira na kukuza mzunguko wa biashara.
Aidha Mhandisi Kavishe ameomba taasisi za kifedha kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na makampuni ya ndani kupata mikopo ili kupanua uwigo wa uwekezaji kwa maslahi mapana ya umma.



