Serikali yakusanya bil 192/- biashara mtandaoni

DODOMA; KAMPUNI 1,820 zimesajiliwa na kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025 serikali imekusanya Sh bilioni 192.78 kutoka kwenye biashara mtandao.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alitoa taarifa hiyo akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Rita Kabati (CCM) aliyetaka kufahamu kama serikali inatambua biashara ya mtandao. Alitaka kufahamu pia idadi ya kampuni zilizojisajili na mapato katika biashara hiyo.
“Serikali inatambua uwepo wa biashara ya mtandao. Kwa sasa kuna jumla ya kampuni 1,820 zimesajiliwa, ambapo kampuni 1,075 biashara mtandao ni shughuli yao kuu na kampuni 745 biashara mtandao ni shughuli nyingine,” alisema.
Kwa, sasa serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu za kuwa na mfumo madhubuti utakaosimamia biashara hizo ambazo zimeanza kuzaa matunda.
“Mfano, kwa kipindi cha Julai, 2024 hadi Machi, 2025 serikali ilikusanya kiasi cha Sh bilioni 192.78 kutoka kwenye biashara mtandao ambayo inajumuisha betting (michezo ya kubashiri) ya mtandaoni,” alisema.
Ili kuhakikisha tunaenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwenye biashara, serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa biashara mtandao ambao upo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wake.
Maeneo yatakayofanyiwa kazi katika utekelezaji wa mkakati huo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Tehama, uboreshaji wa sera, sheria na kanuni na uboreshaji wa huduma za mawasiliano, usafirishaji na uchukuzi.
Mengine ni uimarishaji wa huduma za miamala kwa njia ya mtandao na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu biashara mtandao ili waweze kutumia mitandao iliyopo kufanya biashara.
Wakati huo huo, katika swali la nyongeza, Rita alitaka kufahamu mkakati ya serikali ya kuzuia udanganyifu na utapeli kwenye biashara za mtandaoni kwani watu wengi wamekuwa wakilizwa kutokana na biashara hiyo.
Kigahe alithibitisha kuwapo changamoto nyingi ambazo serikali ilikuja na mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Biashara ya Taifa 2003 toleo 2023.
Alitaja mikakati mingine kupitia wizara mbalimbali akitoa mfano wa Wizara ya Fedha yenye kitengo cha kusimamia biashara mtandaoni kuhakikisha mapato yanaongezeka kwa kufuatilia na kuona biashara hizo zinalipiwa kodi.



