Mambo yanoga kiwanda cha kisasa uchapaji TSN

DODOMA; KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN), imetekeleza ufungaji wa mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji na mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2025/26.

“Mradi unahusisha ununuzi wa mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji, ujenzi wa jengo la kiwanda cha uchapaji, ununuzi wa malighafi za kiwandani na ununuzi wa vitendea kazi ikiwamo magari.

“Hadi Aprli 2025 utekelezaji wa ujenzi wa jengo la kiwanda cha uchapaji umefikia asilimia 53, ununuzi wa mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji umefikia asilimia 80 na ununuzi wa vitendea kazi ikiwamo magari umefanyika.

“Aidha, mpaka kufikia Aprili 2025 TSN imepokea Bilioni 18.2 ambapo mradi huo unategemea kukamilika Septemba 2025.

“Mheshimiwa Spika, TSN katika kuhakikisha habari zinawafikia umma imetekeleza jukumu la kuchapa nakala ngumu za magazeti ya Daily News na HabariLEO ambapo hadi kufikia Aprili 2025 jumla ya nakala za magazeti 1,903,500 zilichapishwa na kusambazwa. Nakala 1,197,000.00 za gazeti la Daily News na nakala 706,500.00 kwa gazeti la HabariLEO.

“ Sambamba na hilo TSN imeendelea kutumia njia ya kidijiti kufikisha habari kwa umma ikiwamo; Gazeti mtandao (e-Paper) kwa kuchapa gazeti tepe la Daily News, HabariLEO na SportLEO, Channel ya Online (Daily News Digital) na kutumia mitandao ya kijamii,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button