Takukuru Iringa yawahoji watia nia CCM

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa imesema imewahoji makada mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotafuta nafasi za ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, kufuatia tuhuma za ukiukwaji wa kanuni za chama na matumizi ya fedha kushawishi wapiga kura.

Akizungumza na wanahabari leo, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Evarist Shija, alisema taarifa za waliohojiwa tayari zimewasilishwa kwa mamlaka za uteuzi ndani ya chama hicho kwa hatua zaidi.

“Nachoweza kusema ni kwamba tumepokea malalamiko mengi kuhusu baadhi ya watia nia wanaodaiwa kuvunja taratibu kwa kutumia fedha kujipatia uungwaji mkono wa kisiasa kabla ya kura za maoni,” alisema Shija.

Amewataka wananchi kuendelea kuipa ushirikiano Takukuru kwa kutoa taarifa ya mipango au matukio yoyote yanayohusu rushwa katika mchakato mzima wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika taarifa yake, Shija pia alieleza mafanikio ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, ikiwemo kusaidia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuongeza mapato yake kwa zaidi ya Sh milioni 105 kupitia ufuatiliaji wa ukusanyaji wa ushuru kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.

Kwa mujibu wa Shija, TAKUKURU ilifanya uchambuzi wa mifumo ya ukusanyaji mapato, kisha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ilifanya ufuatiliaji katika kata 18 ambapo mapato yaliongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na udhibiti wa mianya ya upotevu wa fedha.

Aidha, alibainisha kuwa taasisi hiyo imekamilisha baadhi ya majalada yanayohusiana na uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha katika ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Iringa, iliyopo wilayani Kilolo.

Shule hiyo iliibua mjadala Julai mwaka jana baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuonyesha kutoridhishwa na thamani ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo, na kuagiza TAKUKURU ifanye uchunguzi, hatua iliyosababisha baadhi ya watumishi kusimamishwa kazi.

Katika ufuatiliaji wake wa miradi ya maendeleo, alisema TAKUKURU Iringa imeshughulikia miradi 22 katika sekta za afya, elimu, maji na mifugo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6.3, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button