Biashara Tanzania, Malawi sasa ioneshe ‘sura mpya’

WIKI mbili za hivi karibuni, HabariLEO Afrika Mashariki lilikuwa na makala zinazohusu uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi na Tanzania na Afrika Kusini ambayo kimsingi, ilikuwa na ‘doa’.

Katika toleo la Aprili 22 hadi 28, 2025, liliandika chini ya kichwa cha habari: ‘Wafanyabiashara Tanzania Wasiwe Yatima Afrika Kusini na Malawi.’ Makala ililaumu kasumba ya wafanyabiashara wa Tanzania kufanywa kama yatima wa kibiashara wanapopeleka mazao ya biashara katika nchi hizo jirani na rafiki za Malawi na Afrika Kusini.

Hii ilikuwa baada ya Watanzania kupata taarifa zisizofurahisha kuhusu nchi hizo jirani na rafiki kujaribu kuvuruga uhusiano wa kibiashara dhidi ya wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuzuia mazao yao kuingia katika nchi hizo.

Kutokana na ‘kichwa na miguu’ ya uamuzi wa nchi hizo kutojulikana, serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ikasema inawasiliana kwa mara ya mwisho na serikali za Afrika Kusini na Malawi ili ziruhusu mazao ya Tanzania yaingie katika nchi hizo.

Akawambia Watanzania kupitia ukurasa wake wa mtandao wa ‘X’ kuwa, uamuzi wa nchi hizo umesababisha wafanyabiashara wa bidhaa za unga, mchele, tangawizi na ndizi kutoka Tanzania kukwama kuingiza mizigo yao katika nchi hizo na kwamba wamezuia mahindi kutoka Tanzania kuingia Malawi.

Aidha, Bashe akaeleza juhudi za miaka mitano za Serikali ya Tanzania kutaka kufunguliwa kwa soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio.

Anasema, “Hii inatukumbusha tulivyohangaika kwa miaka kumi kufungua soko la zao la parachichi mpaka pale tulipoamua kutaka kuzuia mazao yao kuingia kwetu; tunaona mwelekeo ni uleule.” Hatimaye, akatoa msimamo kuwa endapo nchi hizo hazitakuwa zimeruhusu mazao ya wafanyabiashara wa Tanzania kuingia ifikapo Jumatano Aprili 23, 2025,

Wizara ya Kilimo ya Tanzania itazuia mazao yote ya kilimo na bidhaa zote za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi zisiingie Tanzania. Akasema: “Aidha, hatutaruhusu zao lolote kutoka nchi hizi mbili kupita ndani ya nchi yetu iwe kwenda Bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote kama tulivyofanya mwaka jana hadi wakatufungulia.”

Anaongeza: “Kwa kuwa tumekuwa tukiwauzia mbolea, tutazuia mbolea kwenda Malawi.” “Kwa hiyo, natoa notisi hii kama kuna wafanyabiashara wa Kitanzania wana mizigo ya kwenda Malawi kuanzia wiki ijayo (Aprili 23, 2025) kama watakuwa hawajabadilisha msimamo, wasipakie chochote.”

Kama kwamba hiyo haitoshi, katika toleo la Aprili 29 hadi Mei 5, 2025, HabariLEO Afrika Mashariki lina makala isemayo: ‘Biashara Malawi, Afrika Kusini Ilinde Rasilimali, Uhusiano’ (Baina ya nchi hizo na Tanzania). Moja ya aya za makala hiyo inasema: “Si siri, Serikali ya Tanzania ilifikia uamuzi huo wa kutoa muda wa mwisho kwa nchi hizo kwani wafanyabiashara wa Tanzania walikuwa wanateseka katika nchi ambazo ni jirani na rafiki zao kibiashara bila sababu za msingi huku kila kukicha hasara itokanayo na bidhaa zao kukwama ikiongezeka.”

Waziri Bashe akaweka ukweli na uwazi kwa Watanzania kupitia ukurasa wake wa ‘X’ alipoandika: “Ifahamike kwamba kama waziri mwenye dhamana, nimefanya jitihada zote za kuwasiliana na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila kupata majibu yoyote.”

Ndio maana katika makala hiyo ya Aprili 22, 2025 mwandishi anaandika, “Kwa mtazamo wangu, msimamo wa Bashe unapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote hasa wafanyabiashara ambao ndio walengwa na waathirika wakubwa wa hilo linalotokea Malawi na Afrika Kusini na ndio wanaoteseka.”

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Makala ya mwisho ikanukuu ya awali ikisema: “Afrika Kusini na Malawi wasitake kuwanyanyapaa wafanyabaishara wa Tanzania kama vile wanataka kuwaona ni ‘yatima masikini. Lazima Watanzania wajiulize; ‘Kama sisi ni  maskini, mbona wanakuja kwetu.”

Ikaongeza: “Wataalamu wa mambo ya uchumi wanasema uchumi wa nchi hukua inapouza zaidi nje ya nchi kuliko inaponunua kutoka nje ya nchi.” “Kwa msingi huo, nchi inapotaka iuze kwako bila wewe kuiuzia maana yake inakutakia mabaya yaani, ‘wewe ukonde, yeye anenepe’ kiuchumi. Hilo halikubaliki.”

Makala zikasema: “Sikio la kufa halisikii dawa’ na ng’ombe hajui umuhimu wa mkia wake hadi unapokatika.”

Kwanini?
Kwa sababu hata baada ya Tanzania kutoa onyo kwa nchi hizo kuwa endapo hazitarekebisha uamuzi kwa kuondoa zuio hilo ndani ya siku saba, Tanzania nayo itazuia uingizaji wa bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini, nchi hizo ziliendelea kukaa kimya.

Kwa mujibu wa makala, huenda nchi hizo zilidhani Tanzania inatishia kwa ‘maji ya moto yasiyounguza nyumba.’ Ni kweli maana zilipuuza na kuendelea kukaa kimya bila marekebisho yoyote kuondoa zuio hadi ‘thamani ya mkia wa ng’ombe’ ilipoonekana baada ya Tanzania nayo kutangaza marufuku ya mazao ya kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini Aprili 23, mwaka huu.

Kama kwamba hiyo haitoshi, Tanzania ikasitisha usafirishaji wa bidhaa hizo kupitia Tanzania kuelekea Malawi ikiwa ni pamoja na mbolea iliyokuwa itumike katika msimu ujao wa kilimo Malawi.

Hata hivyo, Aprili 26, 2025 Tanzania kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ikatangaza kuondoa zuio hilo la biashara na usafirishaji wa mazao ya kilimo kati ya Tanzania na nchi za Malawi na Afrika Kusini kutoa nafasi kwa mchakato wa kidiplomasia kuendelea.

Kwamba hiyo ilitokana na kuwapo kwa mawasiliano rasmi kutoka nchi hizo na nia ya kutaka majadiliano ya pamoja. Bashe ananukuliwa akisema, “Tunaamini majadiliano yanayoendelea yatatoa suluhisho la kudumu.”

Kuhusu Afrika Kusini, waziri huyo anasema majadiliano kati ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu na mamlaka husika za Afrika Kusini yanaendelea ili kuhakikisha masuala ya afya ya mimea na masoko kwa maslahi ya nchi zote mbili yaani Tanzania na Afrika Kusini yanatakiwa yaani ‘tupate wote’ na si ‘mimi nikuwezeshe kupata, wewe uniwezeshe kukosa.’

Kimsingi, taarifa kuwa majadiliano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na Malawi yaliyofanyika Mei 2, 2025 yamefanikisha makubaliano ya kuendelea na biashara baina ya nchi hizo ni habari njema kwa wapenda uhusiano, biashara na kukua kwa uchumi.

Kwa mujibu wa Tovuti ya Wizara ya Kilimo, tukio hilo muhimu la kibiashara na kiuchumi liliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo kwa upande wa Tanzania na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Nancy Gladys Tembo jijini Dodoma siku hiyo.

Katika tovuti hiyo, Wizara ya Kilimo inasema: “Majadiliano hayo yamehusisha mawaziri Hussein Bashe wa Wizara ya Kilimo na Dk Selemani Jafo wa Wizara ya Viwanda na Biashara za Tanzania.”

Inasema kwa Tanzania, timu za wataalamu ziliongozwa na makatibu wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Samwel Shelukindo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah na Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri.

Kimsingi, kusainiwa kwa Tamko la Pamoja ni uthibitisho wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi kwa bidhaa mbalimbali ikiwemo mazao ya kilimo kadiri ya mikataba na miongozo ya kikanda na kimataifa iliyopo.

Kwa msingi, huo Watanzania wanaupongeza uongozi na msimamo thabiti wa Tanzania kupitia Wizara ya
Kilimo chini ya Waziri Bashe kwa kutetea na kulinda maslahi ya wafanyabiashara wa Tanzania nje ya nchi.
Wanasema kwa hatua hiyo, kila upande ukusudie kufanya biashara sawa na barabara ya njia mbili ili kila upande unufaike na si upande mmoja kutaka kulishwa kwa gharama ya upande mwingine.

Hivyo, baada ya kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa Tanzania na Malawi, sasa biashara baina ya nchi hizi
ioneshe ‘sura mpya’ yenye mwelekeo chanya kunufaisha pande zote maana undugu ni kufaana na si kufanana.

‘Sasa kumekucha na jogoo amekwishawika.’ Watanzania waongeze juhudi na ubora katika uzalishaji, uandaaji na
usafirishaji wa bidhaa zao ili zizidi kushika soko zaidi na kuthibitisha ubora wa mazao ya Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button