Mchengerwa aagiza wamachinga wawe kipaumbele masoko mapya
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameagiza wamachinga kote nchini wapewe kipaumbele masoko ya kimkakati yanayojengwa.
Mchengerwa alitoa agizo hilo juzi kwenye uzinduzi wa soko la nyama choma Vingunguti Dar es Salaam baada ya wamachinga kuomba nafasi kwenye ujenzi wa mji wa kisasa wa Jangwani.
“Maelekezo yangu kwa Katibu (Tamisemi-Adolf Ndunguru) masoko yote ya kimkakati yanayojengwa nchini waelekeze wakurugenzi wote wa halmashauri kuhakikisha wamachinga kote nchini wanapewa kipaumbele kwenye maeneo tunayojenga,” alisema.
Alisema anatambua ujenzi wa Soko la kimataifa la Kariakoo umekamilika, hivyo alimuagiza Katibu Mkuu Tamisemi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakutane na kufikiria uwezekano wa kuwapa nafasi wamachinga kwa namna watakavyokubaliana.
“Jambo la pili kaeni mfikirie namna ya kufanya mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Kariakoo na timu yake na wao wapate ofisi kwenye soko hilo la kisasa,” alisema.
Kuhusu mji wa kisasa wa Jangwani, Mchengerwa alitoa maelekezo michoro iwekwe majengo kwa ajili ya maduka ya wamachinga.
“Michoro mtakayokwenda kuiandaa hakikisheni wamachinga mnawafikiria lazima nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi,” alisema.
Aidha, Mchengerwa aliwataka wakurugenzi wote nchini kutoa kipaumbele kwa makundi ya wamachinga, mama lishe na ofisa usafirishaji (bodaboda) na makundi mengine kuhusu mikopo ya asilimia 10.
“Hakikisheni mnawasaidia na hayo ndio maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu (Rais Samia Suluhu Hassan) hakikisheni mmeyashika na kuyaunga mkono na kutatia moyo ili kesho yawe makundi makubwa yatakayoshiriki katika kulipa kodi na kujenga uchumi wa nchi yetu,” alisema.
Mchengerwa alisema kukamilika kwa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha miradi mingi kama ilivyoahidi.
Soko hilo la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kutoa ajira 232 huku 15 zikiwa za kudumu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Masoko wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Alex Buberwa katika ajira hizo 232, wachoma nyama ni 25, mama lishe 56, wauza vinywaji 26, wauza maduka 42, wauza matunda na mbogamboga 48, wauza vinywaji vya asili 15, wauza vinywaji baridi 14 wakiwemo watoa huduma ndogondogo za kifedha.



