Vijana wajizatiti kilimo biashara cha alizeti

KILIMO cha biashara ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, kilimo hicho kinachoweza kubadili hali ya maisha na kukuza uchumi wa jamii, kinahitaji mipango thabiti, utafiti wa soko na matumizi ya mbinu bora za kilimo.

Tofauti na kilimo cha kujikimu kinacholenga kujitosheleza kwa chakula, hiki ni kilimo kinachofanywa kupata faida kutokana na mauzo mazao au bidhaa za kilimo katika masoko ya ndani au ya nje ya nchi. Kilimo cha biashara hufanywa kwa kuzingatia uzalishaji wa kibiashara kuwezesha mkulima au kampuni kupata kipato cha
ziada.

Kilimo hiki kinaweza kuhusisha mazao ya chakula kama mahindi, mpunga na viazi au mazao ya biashara kama alizeti, kahawa, chai, pamba na tumbaku. Kinahusisha matumizi ya teknolojia, mbegu bora, mbolea, dawa mbinu bora za kitaalamu kuongeza uzalishaji ukiwamo umwagiliaji hasa katika maeneo yenye ukame.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kiuchumi na kilimo cha kibiashara, kilimo hiki huhitaji utafiti wa kina wa soko kuhakikisha mkulima anazalisha bidhaa zenye soko la uhakika na zinalingana na mahitaji ya wateja. Vinasema kabla ya kuanza kilimo cha biashara, ni muhimu kuandaa bajeti kujua gharama za uzalishaji na faida inayotarajiwa.

Kwa kutambua faida ya kilimo biashara katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, umeundwa Mtandao wa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa (MVIHAWIKI) kuendeleza kilimo cha alizeti. Mtandao huo una vikundi 186 vya vijana wanaojishughulisha na kilimo biashara cha la alizeti ili wajikwamue kiuchumi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, serikali imeviwezesha vikundi hivyo 186 vilivyo katika vijiji 11 kupata mashamba watakayoyatumia kuendeleza kilimo biashara kwa mazao mbalimbali hususani alizeti.

Anasema hatua hiyo inalenga kuunga mkono mpango endelevu wa kilimo katika kutekeleza Sera ya Vijana 2024 2034. Shaka anasema katika wilaya hiyo tayari umezinduliwa mradi wa shamba la alizeti lililo chini ya mtandao wa vijana wa Mvihawiki.

Anasema serikali imegawa shamba lenye ukubwa wa ekari 7,4798. 93 lililofutwa na kugawanywa tena kwa vikundi vya vijana vilivyopo katika baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo. Shaka anavijata vikundi vya vijana vilivyopatiwa mashamba kwa ajili ya uzalishaji wa mazao kwa mfumo wa kilimo biashara kuwa ni pamoja na Kwalukwambe,

Chanzuru, Muungano, Ilonga, Mfulu, Msowero, Majambaa, Madudu, Dodoma Isanga na Changarawe. Anasema kupitia vikundi vyao, serikali imewapa vijana hao maeneo ya mashamba kuwawezeshac kutumiza azma yao ya kujiajiri kupitia kilimo biashara.

“Ni miaka mingi uchumi wa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa unategemea kilimo kwa asilimia 75…” anasema Shaka. Anaongeza kuwa, mkakati wa serikali ni kuwezesha wananchi kiuchumi likiwemo kundi la vijana. Anasema kwa Kilosa, vikundi 189 vimegawiwa mashamba wanayotumiwa kwa shughuli za kilimo biashara na kwamba, vijana hao wameonesha njia sahihi.

Katibu wa Mvihawiki, Flora Mgaya anasema vijana 40 kati ya hao 29 ni wanaume na 11 ni wanawake halmashauri ya Wilaya ya Kilosa walioungana kupitia mtandao huo wa Mvihawiki. Kwa mujibu wa Flora, baada ya kuungana vijana hao wameanzisha shamba la alizeti lenye ukubwa wa ekari 20, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwawezesha kiuchumi.

Anasema maandalizi ya shamba hilo yamegharimu Sh milioni 3.72 zilizotolewa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri hiyo chini ya Mpango wa Maendeleo ya Vijana wa Taifa wa Mwaka 2007 na Mkakati wa Utekelezaji wa Miaka 10 (2024–2034).

Flora anasema mradi huu unaunga mkono maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia programu ya Build a Better Tomorrow (BBT), inayolenga kuwainua vijanakiuchumi kupitia sekta ya kilimo.

Anasema katika hatua za awali, mtandao unajishughulisha na kilimo cha alizeti ambacho ni moja ya mazao ya kipaumbele yanayolimwa na wakulima wadogo, vikundi vya vijana, taasisi za serikali na watu binafsi katika kata 39 kati ya 40 zilizopo wilayani Kilosa.

Anasema ekari 27,533 zimetengwa kwa kilimo cha alizeti na tayari ekari 14,594 zimelimwa na kwamba, ekari hizo zinatoa uzalishaji wa takribani tani 8,172 kwa msimu. Ekari moja hutoa wastani wa gunia 8.1 zenye uzito wa
kilo 70. “Lengo la mradi huu ni kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana katika kilimo na kuongeza kipato
kupitia sekta ya kilimo,” anasema Flora.

Kwa mujibu wa watalamu wa kilimo, zao la alizeti lina matumizi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutengeneza mafuta ya matumizi mbalimbali hasa ya kupikia, malighafi ya kulishia mifugo na matumizi ya viwandani. Wataalamu wa afya wanapendekeza matumizi ya mafuta ya alizeti katika mapishi kwa kuwa hayana lehemu na hivyo ni salama kiafya hasa yanapotumika vizuri.

Kwa sababu hiyo mafuta yanayotokana na alizeti yamekuwa na soko zuri na hivyo biashara yake ni njia nzuri ya kumwongezea mkulima na mfanyabiashara kipato. Faida nyingine ni mashudu yanayotokana na alizeti baada ya kukamua mafuta. Mashudu hutumika kama chakula bora kulishia mifugo kama vile ng’ombe wa maziwa, mbuzi, nguruwe, kuku au sungura.

Yana kiasi kikubwa cha protini na mafuta na kiasi cha nyuzinyuzi muhimu kwa mmeng’enyo wa chakula kwa wanyama. Eneo lingine linalotokana na faida ya zao hilo ni mafuta yanayotokana na alizeti pia yanaweza kutumika katika utengenezaji wa sabuni, rangi na vipodozi mbalimbali.

Inaelezwa pia kwamba, viwanda vya kutengeneza karatasi hutumia baadhi ya sehemu za mmea wa alizeti kama malighafi katika utengenezaji wa karatasi.

Kwa mantiki hiyo, Katibu wa Mvihawiki, Flora anasema ili kufanikisha utekelezaji wa programu hiyo kwa vijana wilayani humo wanatarajia kutumia Sh milioni 191.8 kutoka kwenye vyanzo vya serikali kuu, halmashauri ya wilaya, wananchi na vijana.

“Tayari vijana 40 wa mtandao wamepatiwa mafunzo elekezi ya kimkakati katika Chuo cha Kilimo Ilonga (MATI) kuhusu shughuli za uzalishaji wa kilimo biashara na kuratibu masuala ya kiutawala ya kimtandao,” anasema Flora. Flora anasema mtandao huo utakuwa kiongozi kuratibu vijana wengine katika vikundi mbalimbali kuhusu uendelevu na ufanyikaji wa shughuli za kilimo biashara kwa ufanisi zaidi.

Kwa mujibu wa Flora, lengo lingine ni kuwa na Saccos kubwa ya vijana kutoka sekta ya kilimo. Anasema mkakati mwingine ni kuunda ushirika imara utatakaonunua alizeti kutoka kwa wakulima wengine ili kufikia soko la uhakika.

“Sisi vijana wasomi tutakuwa mabalozi wa kubalilisha mitazamo potofu ya vijana ambao hawaamini kuwa kilimo ni biashara na kinalipa…” anasema Flora.

Flora anasema kwa awamu ya kwanza, mpango huo unalenga kufikia vijana zaidi ya 1,000 ifikapo Juni 2026. “Tunalenga kuongeza vijana ili wengi waweze fursa hizo katika mfumo rasmi wa ajira zenye staha kupitia kilimo biashara,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button