Kagera wapania kuinua uzalishaji kahawa

MKOA wa Kagera ni miongoni mwa maeneo yenye historia ndefu ya kilimo cha kahawa, zao ambalo kwa sasa linaendelea kuchangia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni kwa taifa.

Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha kahawa kutoka inayolimwa Kagera imekuwa ikivutia soko la kimataifa na kuchangia kiasi kikubwa cha mauzo ya nje.

Inaelezwa kwa msimu wa 2024/2025 kahawa ya Kagera imechangia asilimia 60 ya kahawa yote liyouzwa nje na kuingiza Sh bilioni 256. Pamoja na mafanikio hayo bado mwitikio wa vijana mkoani humo kushiriki kilimo cha kahawa ni mdogo jambo ambali linawakosesha fursa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amekuwa na malengo na shauku ya kuona akikuza ajira kwa vijana kupitia kilimo cha kahawa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Mwasa anasema Kagera sio masikini na anaamini mipango mizuri ikiwekwa kwa mkoa huo katika kilimo cha kahawa unaweza kutoka kupata Sh bilioni 250 hadi bilioni 900 ifikapo 2030.

Anasema hilo litawezekana ikiwa kila kaya itashiriki katika kilimo cha kahawa pamoja na kuweka mikakati ya kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo hicho.

Anasema Serikali ya Tanzania kupitia Sera ya Taifa ya Kilimo (2013) inatambua umuhimu wa kushirikisha vijana katika sekta ya kilimo na Mpango wa Maendeleo wa Kilimo kwa Vijana (NAIVS, ASDP-II) pia unalenga kuwajengea vijana uwezo na kuwavuta kutumia teknolojia katika kilimo.

Mwasa anasema kama malengo ya serikali na sera ni kuongeza tija, kuondoa umasikini na kuongeza ajira kwa vijana na ikiwa kahawa mkoani Kagera imepanda bei kutoka Sh 1,200 ndani ya miaka michache na kuvuka Sh 5,000 hakuna kikwazo tena cha kuzuia vijana kushiriki kilimo cha kahawa.

Kupitia Mkutano Mkuu wa Wadau wa Kahawa uliofanyika hivi karibuni, anasema serikali imekuwa ikifanya juhudi za kutafuta masoko na kupandisha thamani ya zao hilo, hivyo hakuna sababu ya vijana kuhofia kushiriki kilimo cha kahawa.

Anasema ziko sababu mbalimbali zinazofanya vijana wasishiriki kilimo cha kahawa na ndizo wanazopaswa kupambana nazo ili kuhakikisha vijana wanajiajiri kupitia kilimo kwani ni zai himilivu linaloweza kudumu hata miaka 100 baada ya kuanza kutoa maua.

Anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja mtazamo hasi kwa vijana wengi ambao wanaona kilimo ni kazi ya watu wasiofanikiwa au wazee na kuongeza kuwa mara nyingi ripoti anazopokea kutoka kwa vyama vya msingi zinaonesha kuwa vijana wengi hawapeleki kahawa.

Anasema kwa muda aliokaa Kagera amejifunza kuwa vijana wengi wanakabiliwa na ukosefu wa mitaji na rasilimali za kuanzisha mashamba au kupata pembejeo hivyo mkoa umekuja na utatuzi huo ili kuongeza ushiriki wa vijana watakaojiajiri kupitia kilimo.

“Moja ya mikakati mikubwa ni kuanzisha Block Faming kama tulivyoanzisha Muleba, mkoa unatarajia kuanzisha ekari 10,000, kwa njia hiyo tunaamini mkoa utapata tani 200,000 kwa msimu hadi kufikia mwaka 2030 na tayari tumeanza kubaini maeneo kila halmashauri na tutaifanyia kazi hivi karibuni,” anasema Mwasa.

Anasema kuwa vijana wengi wanavutiwa na ushindani wa ajira za mijini na maisha ya mijini wakiamini ni yenye mafanikio zaidi na wengi huangukia kuendesha bodaboda kwa tamaa za fedha ya harakaharaka lakini hakuna anayewaza akizeeka ataenda wapi au atafanya nini na watoto wake watarithi nini.

Anawataka wadau wa kahawa watazame upya ukosefu wa elimu ya kilimo biashara kwa vijana ili kuwapatia ujuzi wa namna ya kuendesha kilimo biashara. Mmoja wa wadau wakubwa wa kuzalisha kahawa mkoani Kagera,

Alberth Katagira anasema kuwa ili kufikia ndoto hizo ni vyema vijana wakapata mafunzo kwa vitendo kama ilivyo mpango wa mkoa wa kutenga mashamba darasa na mafunzo ya kuonesha faida za kilimo cha kahawa kwa vitendo na jambo ambalo litavutia vijana kuliko ilivyo sasa.

Naye Lawrance Ndibalema anasema kuanzishwa kwa teknolojia na ubunifu pamoja na programu za kidijiti kwa kilimo (programu tumizi za bei, soko na ushauri) inaweza kuwa msaada mkubwa kwa vijana wa kisasa wanaochukulia kilimo kama ugumu wa maisha.

Anasema jambo lingine ni Ushirikishwaji kwenye vikundi vya ushirika na kama kuna vikwazo vibainishwe ili vijana wapewe nafasi ya kujiunga au kuunda ushirika wa vijana.

Mzalishaji wa miche ya kahawa, Amina Kashoro anasema ni vyema njia bora za kuvutia vijana zikawekwa kama maazimio ili zitekelezwe na wadau wa kahawa wanapaswa kuweka mazingira wezeshi, kupitia sera, sheria na miundombinu bora (barabara, masoko, zana).

Anasema serikali za vijiji zinapaswa kuwezesha upatikanaji wa ardhi ili vijana wengi hasa wasio na ardhi wapate
maeneo ya kuanzisha kilimo.

Anashauri kuwe na mpango maalumu wa vijana kwenye kilimo cha kahawa kama vile mfuko wa kahawa kwa vijana au ‘Kagera Youth Coffee Fund’ pamoja na Mashindano yanayoambatana na tuzo za kilimo bora kwa vijana Ili kuongeza motisha na kuhamasisha ushindani chanya.

Meneja wa Bodi ya Kahawa mkoani Kagera, Edmond Zan anasema ili Mkoa wa Kagera uondokane na umasikini na kutumia kikamilifu fursa ya kahawa, vijana ni lazima wawe sehemu ya mabadiliko.

Anasema Serikali, jamii na wadau wanapaswa kushirikiana kwa vitendo kuwavuta vijana kwenye kilimo hicho cha kimkakati, kwa kuwa kilimo cha kahawa si tu ni chanzo cha ajira, bali ni njia ya kujenga uchumi imara wa mkoa na taifa.

Mmoja wa vijana wachache wanaofanya kilimo cha kahawa, Dauson Byeyanga anasema vijana wengi wanasumbuliwa na hofu lakini anaamini mipango iliyowekwa inaweza kumuondoa kijana kwenye umasikini na endapo vijana watakubali kushauriwa Mkoa wa Kagera utatajirika kupitia kilimo cha kahawa.

Anasema haikuwa rahisi kwake kujitosa katika kilimo hicho ila baada ya serikali kupandisha bei aliona ni moja ya fursa muhimu ya kumuondoa katika umasikini na aliamua kuachana na shamba la urithi na kuanza na shamba jipya ambalo litaanza kutoa matunda msimu huu.

Anasema vijana wengi wanatakiwa kuondolewa hofu na kuelezwa kwa mifano halisi na kwamba yeye mfano hali na anajivunia vijana wenzake ambao wameanza kuungana naye kwa kumfuata kupata ushauri kwake na kuanza kilimo cha kahawa.

Kijana kutoka Wilaya ya Missenyi, Respikius John ambaye amekuwa akiongozwa na kaulimbiu ya utajiri uko shambani, anasema mara nyingi amekuwa akiwaambia vijana wasichoke kujaribu kujiajiri kupitia kilimo kwani anaamini moja ya nia ya serikali ya kuongeza bei ni pamoja na vijana kujiajiri kupitia kilimo cha kahawa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button