Wananchi 400 kunufaika mradi usimamizi fedha

DAR ES SALAAM: JUMLA ya wananchi 400 watahusishwa katika  mradi wa “Raia Makini Project”unaohusu kuwajengea  uwezo wa  usimamizi bora wa fedha za umma kwa kuwashirikisha kupata taarifa na uelewa mpana wa masuala ya uwajibikaji.

Mradi huo wa miezi 30 utakaogharimu Sh Bilioni 3.3 unaendeshwa na Taasisi ya WAJIBU Institute of Public Accountability na Policy Forum unalenga kumfanya mwananchi kujielewa,kushiriki, kufuatiliaji, kuwajibikaji na kuchukua hatua.

Akizungumza jijini Dodoma leo  wakati wa kufungua mafunzo kwa waandishi wa habari,asasi za kiraia na maofisa wa serikali,Mkurugenzi wa WAJIBU, Ludovick Utouh amesema kati ya watu 400 watu 300 watatoka mikoa ya Tanzania bara na watu 100 kutoka visiwani Zanzibar.

“Mradi huu unalenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa fedha za umma,utaandaa na kusambaza taarifa muhimu kwa lugha rahisi kuhusu usimamizi wa fedha za umma, huku ukiwawezesha wadau wa uwajibikaji kuhamasisha uwazi na uwajibikaji wa Serikali.

Aidha amesema mradi utaimarisha ushirikiano kati ya AZAKI, vyombo vya habari na wananchi kwa kushirikiana na viongozi kufanya maamuzi kupitia majukwaa rasmi ya majadiliano katika ngazi ya kitaifa na kiwilaya.

Utouh ameeleza kuwa malengo  matatu ya mradi ni kuzalisha na kusambaza taarifa kwa lugha rahisi  kwa ajili ya kuwawezesha wananchi na wadau wasio wa serikali kushiriki kwenye mijadala ya umma na midahalo ya sera, na kushawishi mageuzi ya sheria na kuimarisha wa mifumo.

“Kuimarisha uwezo wa wadau wa uwajibikaji kuhusu usimamizi wa fedha za umma ili waweze kushiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa wenye mamlaka katika ngazi ya kitaifa na za wilaya.

Ameongeza “kukutanisha asasi za kiraia, vyombo vya habari, na wananchi ili kushirikiana na viongozi wa maamuzi katika kuhamasisha uwazi na uwajibikaji kwenye usimamizi wa fedha za umma, ukusanyaji wa rasilimali za ndani, na mapambano dhidi ya rushwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Policy Forum ,Semkae Kilonzo amesma wameona ni busara kuunganisha nguvu kuomba mradi  huo ili kufanye kazi na anafarijika  kwasababu tayari wanaanza kuchanja mbuga.

“Niwapongeze sana kupata hii fursa tujengeane uwezo nawashukuru wadau wetu Umoja wa Ulaya (EU) na wengine tutaeleza matokeo tutakayoyapata katika mradi huu,”amesisitiza.

Naye Naibu Mkaguzi Mkuu na Mwakilishi wa Mdhibiti na  Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Wendy Massoy amesema mradi huo utarahisisha kazi za CAG kwa wananchi kujua haki zao na watatoa ushirikiano kwa taarifa za CAG.

“Huu ni mradi mzuri utaongeza tija na uboreshaji wa usimamizi wa mali ya umma na watu wakijua haki zao wataripoti matukio yasiyofaa kama ukwepaji kodi na hata mali ya umma inayosimamiwa vibaya ,”amesisitiza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button