“Wananchi changamkieni fursa nishati safi”

DAR ES SALAAM: Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ili kujiongezea kipato sambamba na kuhifadhi na mazingira na kulinda afya.
Mhandisi Mwandamizi, Deusdedit Malulu kutoka REA ametoa wito huo Mei 28, 2025 Jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Wiki ya Nishati Jadidifu aliposhiriki katika mjadala kuhusu nafasi ya nishati jadidifu katika kufikia lengo la taifa la kufikia 80% ya wananchi kutumia nishati hiyo ifikapo 2034.
“Tunatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, nataka niwaeleze wananchi wenzangu fursa ni nyingi sana katika mnyororo mzima wa nishati safi, tuchangamkie,”…Alisisitiza alisisitiza Mha. Malulu.
SOMA ZAIDI: REA waendelea kuhamasisha matumizi nishati safi
Amesema mwitikio wa wananchi katika kutumia nishati safi ya kupikia ni mkubwa na kwamba mnyororo wake ni mpana hivyo fursa zilizopo ni nyingi ambazo wananchi wanaweza kunufaika nazo.
“Tunafarijika kuona wananchi wanaendelea kuelimika na kuhamasika kutumia nishati safi ya kupikia kwani tayari wameona faida zake,” amesema.
Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaendelea kuwezesha miradi ya nishati safi kote nchini hivyo ni suala la mwananchi kutazama wapi anaweza shiriki na namna bora ya kushiriki katika mnyororo huo wa thamani.
SOMA ZAIDI: Mkakati nishati safi ya kupikia wapata mafanikio makubwa
Aidha, katika hatua nyingine Malulu aliongeza kuwa Serikali imetenga fedha nyingi ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kuwezesha miradi na kwamba REA inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo sambamba na kutoa uwezeshaji kwa namna mbalimbali ikiwemo ruzuku kwenye baadhi ya bidhaa ikiwemo majiko banifu na mitungi ya gesi ya kilo 6.



