Mil 38/- zarejeshwa makundi maalum Rukwa

RUKWA: TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Rukwa imefanikisha kurejesha zaidi ya Sh milioni 38 ikiwa ni sehemu ya mikopo ya makundi maalumu iliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Rukwa, Mzalendo Widege amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025 taasisi hiyo ilifanya uchambuzi wa mfumo wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa makundi maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Aidha, utafiti huo ulibaini kuwa kiasi cha Sh zaidi ya milioni 224 hakikurejeshwa na baada ya ufuatiliaji kiasi cha Sh milioni 38.5 kilirejeshwa ambapo ufuatiliaji wa kiasi cha kilichobaki cha Sh milioni 186.4 bado unaendelea.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho taasisi hiyo ilifuatilia utekelezaji wa miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya Sh milioni 268 ili kubaini ubora na thamani ya fedha ya miradi hiyo ambapo mapungufu yaliyobainika yalitolewa na ushauri na kurekebishwa.
“Tumefanikiwa kutoa elimu ya madhara ya rushwa katika jamii pamoja na athari za rushwa kwenye uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 katika vijiji vya Mwazye, Kalasasi, Mombo na Chipapa.
Tumefikia wana klabu wa klabu za wapinga rushwa 74 katika shule za msingi na sekondari pia tumefanya semina 26,” amesema.
Aidha, kupitia Programu ya Takukuru Rafiki, taasisi hiyo ilipokea kero 102 kutoka Kata 16 ambapo kero 48 zimeshughulikiwa.
Pia imepokea malalamiko mbalimbali 79 ambapo taarifa zilizohusu rushwa zilikuwa 29 na zisizohusu rushwa 50 huku mikakati ya Aprili hadi Juni mwaka huu ni kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi mkuu, sifa za kiongozi anayestahili kuchaguliwa na madhara ya rushwa kwenye uchaguzi.
Katika hatua nyingine kwa upande wa uchunguzi wa mashtaka kesi 13 zinaendelea mahakamani ,kesi mpya ni sita zilizoamuliwa ni mbili huku zilizoshindwa ni mbili.



