Wakalimani 300 lugha ya alama wajisajili
DODOMA; SERIKALI imesema wakalimani 300 wa lugha ya alama tayari wamejisali kwenye kanzidata ya wakalimani wa lugha hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Ikupa aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuifanya lugha ya alama kuwa lugha rasmi ya mawasiliano.
“Serikali inaitambua lugha ya alama kama mojawapo ya lugha rasmi za mawasiliano miongoni mwa wenzetu wenye changamoto ya usikivu hafifu.
“Aidha, Kanuni za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) za mwaka 2019 Kifungu cha 34 (1-3) na 35 (1-3) vinaeleza namna bora ya usimamizi na uendeshaji wa Ukalimani wa Lugha ya Alama ikiwa ni pamoja na kuunda kanzidata ya wakalimani wa lugha hiyo na kuratibu utumiwaji wao katika shughuli mbalimbali za kiserikali na kijamii.
“Mkakati wa Serikali ni kusaidia ukuaji na weledi katika taaluma hii kwa kuwapatia mafunzo ya msasa yatakayowasaidia kuwa wakalimani bora na wanaoweza kutumiwa ndani na nje ya Nchi.
“Halikadhalika, kupitia Kanuni hizo tayari kanzidata ya wakalimani wa lugha hiyo imeanza kuundwa ambapo zaidi wakalimani 300 wamejisajili na hatua inayofuata ni kuwapa mafunzo na kubainisha wale wanaokidhi vigezo.
“Vilevile, muundo wa Utumishi wa kada hii tayari umeandaliwa. Hatua nyingine zilizopangwa na Serikali ni pamoja na kuwawezesha wale watakaokidhi vigezo kujifunza pia alama za kimataifa ili waweze kutumiwa ndani na nje ya Tanzania,” amesema Naibu Waziri.



