Ggml yaongeza nguvu kuing’arisha Manispaa ya Geita

GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imezindua kampeni maalum kuunga mkono kampeni ya usafi wa mazingira hususani kwenye maeneo ya mikusanyiko katika Manispaa ya Geita.
Kampeni hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo huadhimishwa Juni 05, ya kila mwaka ambapo GGML imeshiriki kwa kutoa vikusanyia taka vyenye thamani ya Sh milioni sita.
Ofisa Mazingira GGML, Justine Fuime ametoa taarifa hiyo Juni 03, 2025 kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo iliyotanguliwa na usafi wa mazingira kwenye maeneo yanayozunguka soko la Nyankumbu mjini Geita.
Justine amesema Kampeni ya GGML inahusisha utoaji wa vifaa vya usafi wa mazingira, vifaa vya kuhifadhia taka, kushirki usafi na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi na wafanyabiashara.
“Hili sio suala la siku moja bali litakuwa ni suala endelevu, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wadau wote ikiwemo ili kufanya maeneo yetu yaweze kuwa safi na salama.
“Suala la usimamizi wa mazingira ni mtambuka kwani linahusisha sekta zote ikiwemo serikali na wadau mbalimbali na asasi za kiraia, na sisi tunafanya hivi kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii” amesema.
Ofisa kutoka Idara ya Mahusiano Mgodi wa GGML, Elibariki Jambalu ametaja miongoni mwa vifaa walivyofadhili ni matenki ya 12 ya kuhifadhia taka, matoroli ya kubebea taka, mafyekeo na mifagio.
“Kutoa vifaa hivi maana yake sisi kama GGML tunajaribu kuhakikisha kwamba shughuli za usafi wa mazingira zinakuwa endelevu na zinafanyika kwa ufasaha” amesema Elibariki.
Ofisa Mazingira Manispaa ya Geita, Sebastian Masunga amekiri kampeni ya GGML itachochea ufanisi wa kampeni ya usafi wa mwisho mwa mwezi na kuongeza hamasa ya wadau wote kushiriki zoezi la usafi.
Amesema manispaa imeweka utaratibu mzuri kwa kampuni ya usafi iliyopewa tenda kuhakikisha inawajibika kukusanya taka nyakati zote kwenye maeneo ya mkusanyiko kuepuka mlundikano wa taka.
Mwenyekiti wa Soko la Nyankumbu mjini Geita, Mchele Mhangwa amesema kampeni ya GGML na Manispaa itawasadia kufanya biashara katika mazingira rafiki na kuepuka magonjwa ya mlipuko.



