Tanroads wapata tuzo uhifadhi mazingira

DODOMA; Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imepata tuzo ya Uhifadhi wa Mazingira kutokana na mchangao wake katika kupunguza gesijoto nchini.
Tuzo hiyo imekabidhiwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani yaliyofajika jijini Dodoma.
TANROADS imepewa tuzo hiyo kutokana na mchango wake wa utunzaji mazingira hususan katika utekelezaji wa ujenzi wa barabara za juu (Fly Over) na mradi wa ujenzi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT), miradi ambayo imetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza gesijoto nchini.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa Mazingira na Jamii wa Wakala huyo, Maharani Madayi aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutambua mchango wa TANROADS katika utunzaji wa mazingira, ikiwemo upandaji wa miti ili kupunguza gesijoto.
“TANROADS itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kutunza mazingira kwa kupunguza gesijoto kwa kupanda miti kandokando ya barabara zilizochini ya wakala,” amesema.
Akihutubia kilele cha maadhimisho hayo, Dk Mpango ameelekeza wizara, taasisi na mamlaka zote za Serikali kuhamasisha na kuelimisha jamii umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza gesijoto nchini.



