Manufaa lukuki ushiriki wa Tanzania maonesho Japan

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan.

Yalianza Aprili 13, 2025 na yanatarajia kumalizika Oktoba 13, 2025. Hii ni mara ya pili kwa Japan (Osaka) kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ya kimataifa. Mara ya mwisho yalifanyika 1970 (EXPO 1970). Pamoja na mambo mengine, Tanzania inatumia maonesho hayo kama fursa kunadi vivutio mbalimbali vilivyopo nchini vikiwemo vya utalii na uwekezaji.

Mamilioni ya watu kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kuyatembelea na hali itakayoliwezesha taifa hili kutangaza zaidi vivutio lukuki vya utalii na uwekezaji sambamba na uwepo mazingira rafiki na salama ya uwekezaji, biashara na utalii.

Katika maonesho yaliyombatana na Siku ya Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan anasema ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika nyanja za kidiplomasia, kiuchumi, kibiashara, kisiasa na kijamii unazidi kuimarika.

Anasema Watanzania watumie maonesho hayo kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Japan na ulimwenguni kwa ujumla kuwekeza Tanzania na hivyo, kukuza uchumi na kuongeza upatikanaji wa ajira.

Anasema kutokana na mabadiliko makubwa ya kisera yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya uwekezaji na biashara na kuondoa urasimu, Watanzania hawana budi kutumia fursa hiyo kuvinadi vivutio hivyo.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Wajapan wanavutiwa na bidhaa nyingi zinazotoka Tanzania zikiwemo chai, kahawa,  ufuta, tumbaku, tingatinga, vinyago, katani, viungo kama karafuu pamoja na madini mbalimbali yanayopatikana nchini. Mauzo ya biashara kati ya Tanzania na Japan yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni saba mwaka 2023 hadi bilioni 37 kwa mwaka 2024.

Waziri Mkuu anawakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na duniani kote kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya elimu, afya, miundombinu, nishati, kilimo na utalii. Anasema hii ni kwa kuwa Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ina amani na utulivu mambo yanayoweka uhakika wa usalama wa uwekezaji na biashara zao.

“…Tanzania licha ya kuwa na fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi yenye rutuba, amani na mazingira tulivu, pia ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa kuwa inapakana na nchi saba,” anasema.

“Hizo ni Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia, Malawi na Msumbuji hivyo kuwawezesha wawekezaji kupata masoko ya uhakika katika mataifa hayo,” anaongeza.

Waziri Mkuu aliyeambatana na viongozi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zainzibar wakiwemo mawaziri, manaibu waziri na wakuu wa taasisi mbalimbali anasema serikali ipo katika mchakato wa kuvifanyia maboresho viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu Sabasaba vilivyopo Dar es Salaam ili viwe na hadhi ya kimataifa zaidi.

Hali hiyo itawezesha kufanyika mikutano na maonesho ya biashara ya kikanda na kimataifa. Mei 26, 2025 katika maonesho hayo, Majaliwa alishiriki Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililohusisha wafanyabiashara wa Tanzania na Japan.

Akasema Tanzania itaendeleza mikakati ya kuwaunganisha wafanyabiashara wake na wa mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Japan kunufaika na fursa zilizopo katika mataifa hayo.

Anasema serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kushiriki makongamano mbalimbali ya kimataifa ambayo yamekuwa yakiwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza tija katika biashara na uwekezaji. “Tumewaeleza wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan fursa zilizopo nchini,” anasema.

Anaongeza: “Hii ni mara ya tatu tunakutana na wafanyabara na wawekezaji kutoka Japan. Tayari tumeanza kuona manufaa ya makongamano haya kutokana na kuongezeka kwa biashara kati ya mataifa haya mawili.”

Kwa mujibu wa Majaliwa, hadi Machi mwaka huu kampuni 24 kutoka Japan zilikuwa zimewekeza Tanzania katika miradi mbalimbali yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 42.70 na kuwezesha Watanzania 1,182 kupata ajira.

Anasema licha ya uwekezaji wa kampuni hizo, Tanzania imeendelea kunufaika na ushirikiano wake na Japan kwa kupata misaada katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo na miundombinu.

Akiwa nchini Japan, Majaliwa anashuhudia utiaji saini wa hati sita za ushirikiano ikiwemo ya ushirikiano kuendeleza sekta ya mafuta baina ya Tanzania na Shirika la JGC la Japan.

Hati nyingine ni baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Axcel Afrika kwa ajili ya kukuza uwekezaji nchini. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Suleimani Jafo anasema dhamira ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uwekezaji inazidi kufunguka.

Anahimiza Watanzania kuchangamkia fursa hizo kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla. Anasema serikali inalenga kuendelea kutafuta fursa za biashara, uwekezaji na utalii kukuza uchumi na kuwezesha upatikanaji wa ajira nchini. Kwamba kipaumbele kimewekwa katika sekta za biashara, miundombinu, utalii, uchumi wa
buluu, uwekezaji kwa kuwa Japan imepiga hatua kubwa katika sekta hizo.

Jafo anasema kipaumbele kingine ni kutafuta wawekezaji watakaoshirikiana nao kuendeleza sekta ya kilimo ili kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya kisasa, katika sekta ya madini ni kuyaongezea thamani madini ya kimkakati.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Omar Said Shaaban anasema serikali imejipanga sawia kutumia fursa za uwekezaji zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.

Anasema serikali hiyo imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya uwekezaji ikiwemo ya ujenzi wa mitaa ya viwanda ambapo mmoja umejengwa Mtaa wa Duga Zuze visiwani Zanzibar na eneo la Chamanangwe Visiwani Pemba.

Mbali na miradi ya ujenzi wa mitaa ya viwanda, Shaaban anasema SMZ kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara Zanzibar wameandaa jarida linaloeleza fursa za uwekezaji Zanzibar lililozinduliwa na Waziri Mkuu na kugawiwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan.

Anasema eneo lingine ambalo SMS imejipanga kutafuta wawekezaji ni uchumi wa buluu kupitia mazao ya bahari ikiwemo usindikaji wa samaki ili kuhakikisha unafanyika kisasa zaidi kwa faida ya wananchi na serikali. Fursa nyingine ambayo Watanzania wanatakiwa kuichangamkia ni biashara ya kaboni.

Mei 28, 2025 Tanzania na Japan zimetia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika mpango wa pamoja wa uwekezaji katika biashara hiyo itakayowezesha kampuni za nchi hizo mbili kuwekeza katika biashara ya kaboni nchini Tanzania.

Utiaji saini wa makubaliano hayo ulifanyika Tokyo, Japan ambapo Tanzania iliongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni na Serikali ya Japan ikaongozwa na Waziri wa Mazingira, Asao Keiichiro (Kei).

Katika tukio hilo Masauni anasema makubaliano hayo yanalenga kuimarisha uhusiano kati ya Japan na Tanzania kwa maendeleo endelevu na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yatakayopanua soko la biashara ya kaboni kutoka kwa wawekezaji wa Japan watakaowekeza katika miradi ya biashara ya hiyo itakayoibuliwa nchini.

Anasema Rais Samia Suluhu Hassan anawataka wataalamu kutoka nchi hizo mbili kushirikiana ili kuhakikisha makubaliano hayo yanaenda katika hatua ya utekelezaji.

Tayari Tanzania imeimarisha uwezo wa kitaasisi na kisheria katika usimamizi wa Biashara ya Kaboni ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa kanuni za mwaka 2022 za kuratibu biashara ya Kaboni na imeshaanzisha Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira iliyofanyiwa marekebisho ya 2025.

Awali, Kamishina Jenerali wa World Expo Osaka 2025 kwa Tanzania na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis anasema kongamano hilo ambalo ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya World Expo Osaka 2025 linalenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Japan.

Anasema maeneo yaliyopewa kipaumbele katika kongamano hilo ni katika sekta ya nishati, madini, kilimo, huduma za kibenki, utalii, uwekezaji na afya.

Awali, Meneja Uenezi na Masoko wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Khamis Dunia alisema ushiriki wa Tanzania katika Maonesho hayo yanayoendelea nchini Japan umeiwezesha mamlaka yao kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Zanzibar.

Anasema kitendo cha kushiriki katika mikutano iliyomhusisha Waziri Mkuu, wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan kimempa fursa kuelezea vipaumbele vya uwekezaji vilivyopo Zanzibar vikiwemo vya uchumi wa buluu na utalii jambo ambalo lililowavutia wawekezaji hao ambao baadhi yao sasa wanaonesha nia kuwekeza Zanzibar.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button