CCM Mkoa wa Iringa waridhishwa na uwekezaji wa DP World, SGR

IRINGA: HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imesema imeridhishwa na maendeleo makubwa ya miundombinu na huduma katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa Kampuni ya DP World kwa kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika ziara ya siku mbili jijini Dar es Salaam, wajumbe wa sekretarieti hiyo walitembelea bandari hiyo, kukagua maendeleo ya uboreshaji kwenye magati mbalimbali ikiwemo gati kuu la DP World, na pia kusafiri kwa treni ya kisasa ya SGR kuelekea Dodoma.
Ziara hiyo ililenga kujionea namna miradi ya kimkakati inavyotekelezwa kwa ufanisi na manufaa yake kwa Taifa.
Wakiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, wajumbe hao walipata fursa ya kuona kazi za upakuaji na upakiaji mizigo, matumizi ya teknolojia ya kisasa, pamoja na utaratibu mpya wa kuhudumia meli na mizigo kutoka mataifa mbalimbali.

Akizungumza na ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, alisema uwekezaji wa DP World umeleta tija kubwa katika muda mfupi kwa kuongeza kasi ya ushughulikiaji mizigo, kupunguza mlundikano wa meli na kuongeza mapato.
“Katika kipindi kifupi tangu DP World kuanza kazi rasmi, tumeona ongezeko la mapato ya bandari. Aidha, muda wa meli kukaa bandarini umepungua kutoka siku tano hadi chini ya siku tatu,” alisema Mbossa.

Kwa mujibu wa Mbossa, mikakati ya muda mrefu inalenga kuongeza uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi, kuboresha magati ya upakiaji na kujenga maeneo ya kuhifadhi mizigo ya kisasa (logistics hubs) yakiwemo ya kuhifadhia bidhaa za mbogaboga na matunda kama parachichi na mengineyo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Said Goha, alisema bandari hiyo imekuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kuongeza mapato ya Serikali na kutoa ajira kwa Watanzania, hususan vijana.
“Tunampongeza Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi ya kisera yaliyoleta tija kubwa. Bandari hii sasa inafanya kazi kwa weledi mkubwa na imefungua milango ya biashara na ushindani wa kimataifa,” alisema Goha.
Goha alibainisha kuwa wananchi wa Iringa na mikoa ya nyanda za juu ni mashahidi kwani nao ni sehemu yaj wanafaka wa huduma bora za bandari kupitia mfumo wa reli na barabara.

Wakiwa kwenye ziara ya kukagua miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR), wajumbe hao walielezwa mafanikio ya mradi huo kutoka kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini.
“SGR imesaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani na kuharakisha usafirishaji wa abiria na mizigo. Mapato yameongezeka kutokana na huduma ya treni ya mwendokasi,” alisema Kihenzile.
Aidha, aliongeza kuwa Serikali inaendelea na ukarabati wa reli ya zamani (MGR), ikiwemo kipande cha Kaliua–Mpanda (km 210), ambapo kazi hiyo imefikia asilimia 24.94 ya utekelezaji.
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Mkoa wa Iringa, Joseph Lyata, aliishukuru serikali akisema mapato yanayopatikana kupitia bandari na reli hiyo yanachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na maji vijijini.
“Ni wazi kuwa kila senti inayopatikana hapa inaenda kuongeza nguvu kwenye bajeti ya Taifa. Sisi kama chama tumeridhika kabisa na tutaendelea kuihamasisha jamii kuunga mkono juhudi hizi,” alisema Lyata.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa wajumbe wa CCM mkoa wa Iringa kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, ikiwa ni mwaliko maalum kutoka kwa Mbunge wao David Kihenzile.
Katika ujumbe wao wa mwisho, viongozi hao walisema wataendelea kuwa mabalozi wa maendeleo na kuhimiza wananchi wa Iringa kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu ujao.



