Dk Nchimbi: CCM inathamini maoni kulinda amani

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema CCM inatambua umuhimu wa kulinda amani na utulivu na kamwe haijawahi kupuuza maoni ya Watanzania katika kulinda amani.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Arusha katika uzinduzi wa Jukwaa la Safari ya Mwanamke Mkoa wa Arusha na kueleza kuwa chama hicho kitafanyia kazi kila maoni yanayotolewa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini na kimila kuhakikisha amani inalindwa.
Pia alizungumzia miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani na kueleza kuwa nchi imepata mafanikio makubwa ikiwemo kukamilisha miradi ya kimkakati.

“Kunasiku niliingiwa na utomvu mzito machoni, nilipata msaada wa kuwekewa maziwa ya mama anayenyonyesha nikapona, sasa nimejifunza wanawake si wabinafsi na wanaombea amani ya nchi na watoto wao,” amesema Dk Nchimbi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ambaye jana ameenguliwa kwenye wadhifa huo, Paul Makonda akizungumza katika kongamano alimshukuru Rais Samia kwa kumteua mara mbili, ambapo kwanza alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa na baadaye Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kueleza kuwa hakutegemea kama angeaga wananchi kwenye jukwaa hilo.
“Nawashukuru watu wa Arusha na kama kuna mtu nilimgusa nilikuwa natekeleza majukumu ya kazi yangu kama RC,nitamuomba RC mpya Kenani Kihongosi aje kuendeleza niliyoacha, kwani kazi yangu ilikuwa ni kuunganisha watu na si kuwagawa,” amesema.

Ameshukuru viongozi wa dini kwa kuliombea Taifa na wazee wa kimila, pia aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa kuwa na upendo wa kweli ikiwemo bidii ya kutafuta fedha.
“Nakushukuru Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, wakuu wa wilaya, madereva na walinzi, watumishi wenzangu ikiwemo wananchi na chama cha mapinduzi kwa jinsi tulivyoshirikiana lakini naawambia muimarike na mfanye kazi sana na kusikiliza wananchi,” amesema.



