Mambo 12 ya TMDA miaka minne ya Samia

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), ina jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na udhibiti wa bidhaa za tumbaku.

Katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa gawio kwa serikali kiasi cha Sh bilioni 23.3 na mafanikio mengine kadhaa na hii ni kutokana na kuongezeka kwa bajeti kulikowezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi hivyo kusababisha kutoa gawio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  kwa umma  Machi 19,2025 TMDA imepongeza namna bora ya utendaji kazi wa  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais  Samia huku ikiainisha mafanikio mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na usajili wa viwanda 18 vya dawa, huku  kukiwa na usajili wa viwanda 140 vya vifaa tiba na vitendanishi na hivyo kuchangia katika uwekezaji nchini.

Fimbo anasema  usajili wa bidhaa za dawa,vifaa tiba na vitendanishi umeongezeka ambapo bidhaa za dawa  zilizosajiliwa sasa  ni 8,303 na  bidhaa 3,019 za vifaa tiba na vitendanishi kutoka bidhaa za dawa 1,286 ambapo dawa ni 933 na vifaa tiba na vitendanishi ni 353 mwaka 2021/2022.

“Kuongeza bajeti kumewezesha kuongeza kiwango cha ufanisi wa  kulikowezesha utoaji huduma kwa nzuri kwa wananchi na kuimarika kwa kwa ufuatiliaji wetu katika vituo vyote  na pia tumetoa gawio kwa serikali haya ni mafanikio makubwa kwa kipindi cha miaka minne.

Anasema serikali imewekeza kiasi cha Sh bilioni 15 katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara ili kuwezesha kufanya maamuzi ya kisayansi katika uchunguzi wa dawa,vifaa tiba,vitendanishi na kazi zingine za kimaabara.

Matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika huduma za utoaji vibali ambapo sasa vinatolewa ndani ya saa 24.

 

“Hili limechangiwa na kuimarika kwa mfumo wa kielektroniki wa utoaji vibali vya kuingiza na kutoa nchini bidhaa unaomwezesha mteja kutuma maombi, kulipa na kupata kibali ndani ya masaa 24,” anasema.

Anasema asilimia 98 ya bidhaa zimeweza  kukidhi vigezo vya ubora na ufanisi na hivyo kuhakikisha usalama wa bidhaa za dawa na vifaa tiba katika soko.

“Lakini pia kuna ongezeko la vituo vya maabara hamishika kutoka 19 hadi 28 ili kuimarisha zoezi la uchunguzi wa sampuli katika maeneo husika,” anaasema.

Mfumo ufuatiliaji madhara ya dawa

Julai 2021 hadi Juni 2022, TMDA imefanikiwa kutekeleza malengo yake ikiwemo kuanzisha mfumo wa kudhibiti madhara yatokanayo na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba kwa watumiaji.

Tangu wakati huo kumekuwa na ongezeko la vituo vya ufuatiliaji wa maudhi ya dawa na chanjo hadi kufikia 30 ili kuimarisha ufuatiliaji wa usalama wa dawa na chanjo nchini.

Fimbo, anasema  ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo, mamlaka imeanzisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ADR Reporting Tool wa utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta na kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi kwenye simu.

Anasema kupitia mfumo huu, TMDA imepokea jumla ya taarifa 4,898 katika kipindi husika na hadi sasa kuna jumla ya taarifa 31,666 kwenye Mfumo wa Taarifa unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ujulikanao kama Vigibase.

Hata hivyo, taarifa hizi ni za maudhi madogo ambayo hayasababishi kuondoa dawa kwenye soko.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Gaudensia Simwanza anasema taarifa hizo hutolewa kwa namba *152*00# baada ya hapo mtu hufuata maelekezo.

“Huduma hii inatolewa bure na mtu anaweza kupata muda wowote. Kwa mfano kuna dawa zinasababisha kichefuchefu, kutapika, usingizi usio wa kawaida, kupata kizunguzungu lakini haya ni madhara yanayotarajiwa kwenye dawa husika na si hatarishi kwa mtumiaji.

“Madhara hatarishi  ni kama vile kubabuka ngozi, kuvimba mwili, kuumwa hadi kulazwa hospitali na hata kusababisha kifo,” anasema Simwanza.

Udhibiti tumbaku

Ili kufanikisha hilo anasema waliandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2021-26) wa Kitaifa wa Kupambana na Tumbaku pamoja na Mpango Kazi wa Miaka Mitano wa Udhibiti wa Tumbaku ambao umeanza kutekelezwa.

“Tumeweka tayari mfumo wa udhibiti wa bidhaa hizi na hadi sasa tumekwishatambua bidhaa zote za tumbaku zilizoko kwenye soko ambapo idadi yake hadi sasa ni bidhaa 51.

Aidha, anaeleza kuwa wameanzisha maabara ya upimaji wa bidhaa za tumbaku kwenye jengo lililoko Dodoma.

Maabara

Aidha, anasema TMDA ina maabara tatu ambazo zimejengwa jijini Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.

“Maabara ya kupima vifaa tiba ya Dar es Salaam imeimarishwa na maabara ya kupima bidhaa za tumbaku iliyoko Dodoma imewekewa mitambo ya kisasa ya upimaji wa bidhaa hizi,” anasema.

Fimbo anasema elimu imeendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mihadhara katika mikoa 23 nchini, kipindi cha televisheni cha TMDA NA JAMIImatangazo ya redioni na kupitia mitandao ya kijamii.

Anaainisha kuwa wameanzisha vilabu 55 vya masomo katika baadhi ya shule za sekondari katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Singida, Dodoma na Mtwara.

Uimarishaji na umaliziaji

Fimbo anasema kutokana na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa katika vituo vya forodha na maeneo ya biashara, mamlaka imeendelea kushikilia vyeti vya kimataifa na kuimarisha maabara zake.

Anasema wataendelea kuimarisha usimamizi wa makusanyo ya maduhuli kutoka vyanzo vya ndani na kutekeleza mkakati wa kuendeleza viwanda vinavyozalisha dawa ndani ya nchi.

Anasema wamekamilisha ujenzi wa miundombinu ya tanuru la kuteketeza bidhaa zisizofaa eneo la Nala mkoani Dodoma ili kuhakikisha bidhaa katika soko ni zile tu zenye ubora, usalama na ufanisi.

Aidha ametaja ongezeko la wafanyakazi kutoka 278 hadi 421 na hivyo kuongeza fursa ya ajira nchini.

” Upanuzi wa ofisi kwa kuongeza sakafu tatu  kwenye jengo la ofisi ya Makao Makuu Dodoma.

Mafanikio zaidi

Anaeleza kuwa TMDA imeendelea kushikilia cheti cha ithibati kwa kiwango cha ISO 9001: 2015 na na Ithibati ya Maabara kwa kiwango cha ISO /IEC 17025:2017 katika utoaji huduma bora baada ya kukidhi vigezo kufuatia kaguzi zinazofanyika kila baada ya miaka mitatu na wahakiki kutoka nje ya nchi.

Anasema wameendelea kushikilia hadhi kwa kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO prequalification) kwa kuwa na mifumo mahiri ya uchunguzi wa dawa.

“Vilevile TMDA ni taasisi iliyohakikiwa na kuweza kufikia ngazi ya tatu kati ya nne (Maturity Level 3) ya WHO ya ubora wa mifumo ya udhibiti wa dawa,” anabainisha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button