Majaliwa ampongeza Rais Samia

DODOMA — Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mafanikio ya Tanzania katika uhusiano wa kimataifa ni ushahidi wa mafanikio ya diplomasia ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Tanzania sasa inaheshimika kimataifa, ikiwa ni pamoja na kushiriki mikutano ya G20, COP29 na majukwaa mbalimbali yanayoweka nchi kwenye ramani ya dunia kisiasa na kiuchumi.
“Maono ya Rais Samia yameiwezesha Tanzania kufikia makubaliano na mikataba muhimu ya maendeleo, ikiwemo ule wa kufufua reli ya TAZARA kwa ushirikiano na China na Zambia,” alisema Waziri Mkuu.
Majaliwa pia aliipongeza Tanzania kwa kuongoza SADC kwenye masuala ya siasa, ulinzi na usalama na kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi za nchi wanachama, jambo alilosema linadhihirisha uaminifu wa kikanda.
Alisisitiza kuwa Tanzania imeimarika kitaifa na kimataifa, hivyo Watanzania wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki katika maendeleo na kulinda heshima ya taifa.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Bunge la 12 limeweka historia kwa kutekeleza majukumu yake kwa kiwango cha juu, ikiwa ni pamoja na kujibu maelfu ya maswali na kupitisha miswada mingi ya maendeleo.
Katika hotuba yake ya kufunga Bunge leo, amesema jumla ya maswali ya msingi 5,259, nyongeza 18,075 na maswali 253 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na kujibiwa, hali inayodhihirisha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi.
“Leo asubuhi, Serikali imewasilisha mezani Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025–2050. Dira hiyo itakuwa zana muhimu itakayotoa mwelekeo wa Taifa kwa miaka 25 ijayo,” alisema Majaliwa.
Aidha, amesema miswada 58, maazimio 922 na mikataba 12 ya kimataifa imepitishwa katika kipindi cha uhai wa Bunge hilo, likiwemo azimio la pongezi kwa Rais Samia kwa uongozi wake wa mfano.
Majaliwa aliwataka wabunge kuwa mabalozi wa utekelezaji wa dira hiyo wanaporudi majimboni ili kuhakikisha wananchi wanaelewa mwelekeo wa taifa kwa vizazi vijavyo.