Kampuni yatoa msaada wa viti zahanati Itezi

MBEYA: KAMPUNI ya Kati Investment imetoa msaada wa viti vinane vya wagonjwa vyenye thamani ya Sh milioni 1.5 kwa Zahanati ya Kata ya Itezi iliyopo jijini Mbeya, lengo kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha miundombinu ya afya inaimarika na wagonjwa kuwa kwenye mazingira bora.

Akikabidhi viti hivyo leo Juni 26, 2025 kwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Eden Katininda, Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Alfred Mwakibete amesema uongozi umeona kuna sababu ya kuunga mkono juhudi za serikali kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga vituo vipya vya matibabu na kuboresha vilivyokuwepo.

Mwakibete amesema baada ya kupokea maombi uongozi wa kampuni ulijiridhisha kuwepo na changamoto ya uhaba wa viti vya kukalia wagonjwa kwenye zahanati hiyo iliyojengwa na serikali.

“Tuliona upya wa zahanati hii tuliyojengewa na serikali unapaswa kuendana na hadhi ya wagonjwa wanaofika kupata utulivu wakati wakisubiri huduma badala ya kusimama au kurandaranda ndani na nje ya jengo,” amesema Mwakibete.

Akipokea msaada huo, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Itezi, Dk Doreen Lyimo amewataja wajawazito kuwa miongoni mwa wateja waliokuwa wakipata wakati mgumu wanapofika kupata huduma na kukuta viti vichache vilivyokuwepo vimekaliwa na wagonjwa wengine.

Dk Lyimo ametaja hitaji lingine lililopo kuwa ni ujenzi wa uzio unaotakiwa kufanyika ili kuimarisha ulinzi wa mali zilizopo kwenye zahanati hiyo.

Baadhi ya wakazi walioshuhudia tukio hilo wakiwemo wagonjwa waliokuwa wamefika kwaajili ya matibabu waliupongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa kuwa na moyo wa kusaidia jamii kwenye mahitaji mbalimbali muhimu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button