UN: Rwanda yatumia teknolojia ya kijeshi kusaidia M23

KINSHASA, DRC: RIPOTI ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Rwanda ina ushawishi mkubwa na mamlaka kwa kundi la waasi wa M23 linaloendesha mashambulizi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rwanda inadaiwa kuwapatia waasi hao mafunzo ya kijeshi, silaha na vifaa vya teknolojia ya hali ya juu vinavyowawezesha kupambana na majeshi ya DRC.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kutokana na usaidizi huo, waasi wa M23 waliweza kudhibiti miji muhimu ya Goma na Bukavu kati ya Januari na Februari mwaka huu, jambo lililowaongezea ushawishi wa kisiasa katika maeneo tajiri kwa madini.

Serikali ya DRC, pamoja na Marekani na mataifa ya Magharibi, wanaituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao kwa lengo la kudhoofisha utawala wa Kinshasa.

Hata hivyo, Rwanda imekanusha tuhuma hizo, ikisisitiza kuwa hatua zake ni za kujihami dhidi ya wanamgambo wa kihutu wa FDLR. SOMA: Rwanda, DRC simamieni mkataba wa Washington kudumisha amani

FDLR ni kundi linalohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda na limekuwa likijihifadhi mashariki mwa Congo kwa miaka kadhaa sasa.

 

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button