Tanzania yang’ara biashara duniani

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Tanzania inang’ara katika biashara duniani.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati akifungua Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam jana.

Alisema maonesho ya mwaka huu yamevutia zaidi ya wafanyabiashara 5,734 kutoka nje na ndani ya Tanzania na hicho ni kielelezo cha mafanikio ya nafasi ya Tanzania kuwa kitovu cha biashara Afrika na duniani kwa ujumla.

Dk Mwinyi alisema katika maonesho ya biashara ya Osaka yanayoendelea Japan, kwa siku wanatembelea watu zaidi ya milioni 5.6 na katika banda la Tanzania waliotembelea ni watu milioni 4.7.

“Kwa mujibu wa Televisheni ya Taifa ya Japan (NHK) tarehe 5 Mei, 2025 ilitangaza Tanzania kuwa mshindi wa pili wa nchi yenye muhuri bora ulioshindanishwa katika mtandao wa Tik Tok ambapo watembeleaji laki tisa na hamsini na mbili elfu waliuchagua. Hongereni sana TanTrade kwa kuendelea kuiweka Tanzania kwenye ramani ya biashara ya dunia,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kiuchumi duniani, Tanzania imeendelea kutekeleza sera na mikakati ya kukuza biashara, viwanda na huduma kupitia wizara za viwanda na biashara Tanzania Bara na Zanzibar kwa kushirikiana na wadau.

Dk Mwinyi amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Mohamed Khamis kwa uongozi wake wa kuijenga taasisi hiyo.

Alisema jitihada zake zimewezesha kuigeuza Tantrade kuwa daraja la mafanikio la kuunganisha na kutangaza sekta zote za biashara ndani na nje ya nchi.

Dk Mwinyi alisema huo ni mfano wa taasisi inayozalisha matokeo yenye tija kwa nchi na yanayoendana na dira ya taifa.

Nembo ya Tanzania

Dk Mwinyi amezindua Nembo ya Tanzania itakayotumika kwenye bidhaa zinazozalishwa nchini ili kutambulika kimataifa katika masoko mbalimbali.

“Nimefurahi kusikia kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kukamilika kwa nembo maalumu ya taifa kwa bidhaa na huduma za Tanzania (Made in Tanzania), ambayo tunaizindua katika maonesho haya,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema hiyo ni hatua muhimu ya maendeleo nchini itakayolitambulisha taifa kimataifa kama taifa lenye bidhaa zenye ubora, ubunifu na fahari ya Kiafrika.

“Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kupenda na kuthamini bidhaa zetu ili kuzidi kuimarisha biashara na viwanda vyetu vya ndani na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu,” alisema Dk Mwinyi.

Aliagiza wizara za viwanda na biashara katika pande zote mbili za Muungano na TanTrade kuhakikisha elimu ya alama hiyo inawafikia wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi.

“Alama hii iwe chachu ya kukuza uzalendo wa kibiashara, kuhamasisha kila Mtanzania kujivunia, kutumia na kutangaza bidhaa zetu,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema serikali zote mbili zimechukua hatua za kimkakati ili kuhakikisha ukuaji wa sekta za viwanda na biashara unakwenda sambamba na dhamira ya taifa ya maendeleo jumuishi.

Alitaja hatua hizo ni pamoja na kurahisisha mazingira ya kufanya biashara, kukuza ubunifu, kushirikiana na sekta binafsi, kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijiti pamoja na kuandaa mifumo ya kutoa maoni na taarifa moja kwa moja ili kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.

 

Aidha, Dk Mwinyi alisema serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi, sekta binafsi, wajasiriamali na wawekezaji katika kujenga mazingira wezeshi ya biashara.

“Niwatake watendaji wote wa umma katika taasisi wezeshi za biashara kuhakikisha wanawezesha ukuaji wa biashara na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika shughuli zote za maendeleo,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button