Ruwa’ich akemea kutegemea sangoma badala ya Mungu

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limekemea watu wanaokimbilia kwa waganga wa kienyeji na sehemu zisizofaa kutafuta ufumbuzi wa changamoto badala ya kumtegemea Mungu.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi alisema hayo wakati wa misa takatifu ya kuwapandisha daraja la upadri mashemasi 11 katika kituo cha Msimbazi Dar es Salaam jana.
Mashemasi hao ni Fransisco Benedicto, George Mbago, Benjamini Maganga, Josephat Mlacha, Gabriel Kiondo, na Mark Clement.
Wengine ni Richard Hazvado, Emmanuel Lazaro, Christian Leonard, Charles Msabila na Kanuth Martin.
Ruwa’ichi aliwataka mapadri hao wasimame imara katika kufanya kazi takatifu ya Mungu bila kulalamika.
“Unaweza kukuta mtu anaenda kwa waganga wote kutafuta ufumbuzi… anakwenda kwa wakorofi na walaghai kutafuta jibu, lakini huko ni kurubuniwa mara nyingi kwani anayetoa uzao ni Mungu si binadamu,” alisema.
Aliongeza: “Ewe shemasi jitambue kama Paulo, Mungu anayekuita sio Mungu wa mizaha ni Mungu anayetaka uthabiti, ukishaitwa ukaitika tukakuwekea mikono na kukupaka mafuta, wewe umeshawekwa wakfu, wewe umetengwa na mambo hovyohovyo na usiruhusu maisha yako kuhusisha mambo yasiyofaa, aibu, kero na chukizo kwa Mungu simama kidete”.
Aliwahimiza wamtangulize Mungu ili awape mwamko wa kudumu katika utumishi wao ulio takatifu ili wawe wakarimu, waaminifu na utayari wa kumtumikia.
Alisema mapadri hao watumie mafundisho ya Mungu kwa kutekeleza huduma takatifu na watambue kwamba wametengwa na mambo maovu.
Aidha, askofu Ruwa’ichi amewapa hati nne ikiwemo ya dara la upadri, hati ya kuwaruhusu kuwaganga watu kwa njia ya Kristu kwa njia ya sakramenti, leseni ya kufungisha ndoa na miongozo inayowahusu mapadri wote wanaofanya utume nchini.
Wakati huo huo ameagiza parokia zote na asasi kujipanga kufanya Novena ya kuombea amani na haki ifikapo Agosti 15 hadi Agosti 23, mwaka huu.
“Baraza la maaskofu limeamua kuwa na siku ya kusali kuombea haki na amani katika nchi yetu na pia tuliomba wanakanisa wote wa Tanzania wawe na siku ya kusali Agosti 23, 2025,” alisema