Majaliwa atoa maagizo makusanyo TRA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuongeza makusanyo.

Majaliwa alisema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Tathmini ya Utendaji wa TRA kilichofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na kukutanaisha watumishi wa TRA kutoka mikoani.

Majaliwa aliielekeza Wizara ya Fedha kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni na TRA zitoe mwelekeo wa kuimarisha makusanyo ili ziboreshwe kufikia wigo wa juu wa kukusanya kodi pamoja na kuwarahisishia watendaji kufanya kazi kwa urahisi.

“Wizara ya Fedha endeleeni kufanya mapitio ya sera zetu kuona kama kuna eneo bado sera yetu haijatufanya tukusanye kodi kwa urahisi tufanye maboresho ya sheria kama wataonesha kwamba sheria hii inatukwaza katika utendaji kazi wetu lakini pia mifumo kanuni ziimarishwe,” alisema.

Pia, ameitaka TRA kuendeleza ubunifu uliosaidia kuongeza makusanyo kwa sababu mbinu zilizotumika zimesaidia kuongeza makusanyo ya mamlaka na kuvuka lengo.

Aidha, Majaliwa aliwataka watumishi wa TRA kuzingatia sheria, utawala bora na utu katika kukusanya kodi pamoja na kuzingatia maadili, uwajibikaji, uzalendo ili taifa lisonge mbele.

Aliitaka TRA kufanya maboresho katika sekta zinazohitaji uboreshaji hasa katika kupunguza wataalamu wa mamlaka na walipakodi kukutana ili kuondoa mianya ya rushwa.

Kuhusu wafanyabiashara wa kigeni kukwepa kodi, Majaliwa alisema ni muhimu wasimamiwe na kutambua sheria za kulipa kodi na TRA ifanye ukaguzi katika ofisi zao mara kwa mara.

Pia, aliitaka sekta binafsi kuhakikisha inatoa elimu kwa wenzao na kuhamasika kulipa kodi kwa hiyari, uaminifu, kwa wakati na kwa maslahi ya taifa akisifu hatua ya ushirikiano iliyofikiwa kwa sasa kati ya wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda na wenye maduka katika kulipa kodi kwa hiyari.

Kwa upande wa wananchi, aliagiza elimu ya mlipakodi kwa hiyari na kufahamu umuhimu wa kulipa kodi kwa manufaa na maendeleo ya taifa.

“Kupitia vyombo vya habari, lazima tuwaambie kulipa kodi ni wajibu ili tujenge miradi tunayoitamani, tuwakumbushe wadai risiti wanaponunua au kupata huduma na wafanyabiashara ni wajibu wenu kutoa risiti,” alisema.

“Tulipe kodi kwa wakati sahihi na kwa uwazi… kodi zote zinarudi kwa wananchi, zinajenga madarasa, barabara na vitu vingine,” alisisitiza.

Kuhusu kuongezeka kwa makusanyo ya kodi, Majaliwa alisema TRA imevuka lengo la kukusanya mapato kwa asilimia 103.9 ya kukusanya Sh trilioni 31.05 kwa kukusanya Sh trilioni 32.26.

Alisema mafanikio hayo yametokana na mabadiliko ya kiutendaji yaliyofanywa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda kwa kufanya maboresho yaliyoongeza mshikamano ndani ya TRA kwa watendaji kuzungumza lugha moja na kufanya kazi kwa pamoja.

Alisema licha ya kuwepo kwa mipango mizuri na usimamizi makini kwa wenye jukumu la kukusanya mapato, TRA imefanikiwa pia kusimamia maboresho ya mifumo, walipakodi na wadau na kuongeza uzalendo, uadilifu na uwajibikaji uliofanya watendaji kutambua wajibu wao.

Aliipongeza TRA kwa kuimarisha mifumo ya Tehama iliyoleta mabadiliko katika kukusanya mapato yaliyowezesha serikali kutekeleza miradi ya maendeleo. Aliwasisitiza kuendelea kuweka mpango kazi utakaovunja rekodi ya makusanyo ya kodi na kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuleta mabadiliko na kukuza uchumi.

Wakati huo huo, Majaliwa alisisitiza umuhimu wa kulinda tunu za nchi hasa amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025.

Alisema wakati wa uchaguzi watakuja watu kutoa ushawishi wa kila aina lakini ni muhimu kuzingatia kuwa haubomoi tunu za taifa

“Fikirieni ushawishi mnaopewa tusikubaliane na mtu anayeleta ushawishi unaotuingiza katika migogoro na kupoteza amani ya nchi,” alisema.

Imeandikwa na John Mhala (Arusha) na Shakila Mtambo (Dar es Salaam).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button