Mwenge waridhishwa na mradi wa ufyatuaji matofali

MANYARA: Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ufyatuaji matofali ya ‘block’ unaotekelezwa na Kikundi cha Wanawake cha Tumaini kilichopo kijiji cha Komolo, wilayani Simanjiro, wenye thamani ya Sh milioni 42.
Mradi huo unaoundwa na wanawake wanane, umeelezwa kuwa umekuwa chachu ya maendeleo kwa kikundi hicho, ambapo kwa siku wanauwezo wa kufyatua matofali 500 yenye ubora unaokidhi viwango.
Akizungumza wakati wa mbio hizo za Mwenge, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake wa Tumaini Komolo, Rukia Dosa, ameishukuru serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kwa kuwawezesha kupata mkopo usio na riba.

Ameeleza kuwa kutokana na ajira hiyo sasa wanawake hao wamesonga mbele kimaisha na hata kuweza kugharamia masomo ya watoto wao bila kutegemea waume zao.
Kwa upande wake Katibu wa kikundi hicho, Zubeda Issa, amewaomba wananchi kuunga mkono juhudi zao kwa kununua matofali wanayozalisha kwa kuwa yana ubora unaotakiwa.
Pia amewahamasisha wanawake wengine kujitokeza na kuanzisha miradi ya kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa na serikali bila riba.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Ismaili Ussi, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kwa kutekeleza ipasavyo agizo la serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu.
Amesema Mwenge wa Uhuru umeridhishwa kwa asilimia 100 na mradi huo, ambao umedhihirisha namna mikopo hiyo inaweza kubadilisha maisha ya wananchi.
Mradi wa Kikundi cha Tumaini Komolo ni mfano wa mafanikio ya utekelezaji wa sera za serikali za kuwezesha makundi maalum kupitia mikopo isiyo na riba ili kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii.



