Dira ya 2025 yaiimarisha nchi

SERIKALI imesema Dira ya Taifa ya mwaka 2000 _ 2025 imeuwezesha uchumi wa nchi kuwa himilivu.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Fredy Msemwa alisema hayo Dodoma jana wakati akitoa taarifa kuhusu kukamilika kwa mchakato wa maandalizi ya Dira ya mwaka 2025- 2050 itakayoanza kutumika Julai mwakani.

Dk Msemwa alisema Dira 2025, ilikuwa na malengo matatu yaliyoiwezesha nchi kupata maendeleo na kusaidia wananchi kupata mafanikio.

“Kwanza kulikuwa na lengo la kujenga uchumi imara na uchumi ambao ni himilivu, kulikuwa na lengo lingine la kuleta maendeleo ya watu pamoja na maendeleo ya jamii, na lengo lingine lilikuwa ni kuongeza ushiriki wa baadhi ya sekta hasa viwanda katika kutoa mchango wa ukuaji wa uchumi katika nchi yetu,” alisema.

Dk Msemwa alisema katika Dira ya 2025 nchi imefanikiwa kujenga uchumi imara wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Wakati Dira ya 2025 inaanza kipato cha mtu mmoja kilikuwa ni dola za kimarekani 457 kwa mwaka na hivi tunavyoongea kipato cha mtu mmoja mmoja ni dola 1300 kwa mwaka, na pato la Taifa limekuwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kule tulipotoka,” alisema.

Aliongeza: “Pamoja na hayo tumefanikiwa kujenga uchumi himilivu kwa maana kujenga uchumi ambao unahimili misukosuko inayotokea ndani ya nchi na inayotokea nje ya nchi”.

Dk Msemwa alisema miaka ya 2020, 2021 Tanzania ilikumbwa na janga la Uviko- 19 na baadaye ukosefu wa dola na vita vya Urusi na Ukraine na nchi nyingi duniani ziliathirika sana kiuchumi.

“Baadhi ya nchi uchumi wao ulikwenda kwenye ukuaji hasi lakini katika kipindi hicho hicho sisi nchi yetu uchumi haukutetereka, ulipungua kidogo kukua, ulishuka ukafika asilimia nne kutoka asilimia sita wakati kuna majirani zetu uchumi wao ulikuwa asilimia moja, kilichotusaidia uchumi wetu usishuke sana ni kwa sababu uchumi wetu hautegemei sekta moja unategemea kilimo cha pamba, kahawa, chai, madini, utalii na uvuvi kwa hiyo hiki kikitetereka hiki kinabadili,” alisema.

Dk Msemwa alisema pia Dira ya 2025 imeleta maendeleo makubwa kwenye huduma za kijamii, elimu, afya maji, usafiri wa nchi kavu, usafiri wa majini na usafiri wa anga.

“Tumepiga hatua kwenye utoshelevu wa huduma za maji, hivi sasa baadhi ya vifaa tiba ambavyo tulikuwa tunavisikia vipo kwenye hospitali moja tu sasa hivi vipo mpaka hospitali ya wilaya, huduma za maji mijini na vijijini, mijini sasa hivi tupo zaidi ya asilimia 90 hadi asilimia 91 tunaelekea asilimia 94, sasa hivi tumeshasogeza umeme katika vijiji vyote tunaelekea kwenye vitongoji vyote, haya ni matokeo ya Dira 2025,” alisema.

Dk Msemwa alisema mchakato wa maandalizi ya Dira ya mwaka 2050 umekamilika na inatarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Dodoma kesho.

Alisema mchakato wa maandalizi ya Dira ya 2050 ulianza Aprili 2023, baada ya serikali kuanzisha Tume ya Taifa ya Mipango iliyoundwa kwa sheria inayoitwa Sheria ya Tume ya Mipango ya Taifa ya Mwaka 2023.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button