Mwinyi afungua jengo jipya la ZEC

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, leo Julai 16, 2025 amezindua rasmi Jengo jipya na la kisasa la Ofisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) lililopo Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha mazingira bora ya utendaji wa taasisi hiyo muhimu kwa demokrasia nchini.
Sambamba na uzinduzi wa jengo hilo, pia Dk Mwinyi amefungua Ofisi ya Wilaya ya Magharibi “B”, na kusisitiza kuwa ujenzi wa majengo hayo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haikusita kugharamia ujenzi wa makao makuu ya Tume hiyo pamoja na ofisi za wilaya, kwa kutambua umuhimu wa taasisi hiyo katika kuhakikisha uchaguzi huru, haki na wa kuaminika.
Kwa mujibu wa taarifa ya kitaalamu, Dk Mwinyi amesema kuwa Serikali imetoa shs Bilioni 14,1 kwa ajili ya mradi huo uliojengwa na kampuni ya ujenzi ya CRJE na kutoa wito kwa watendaji wa Tume hiyo kuzitunza ofisi hizo ili ziendelee kuwa katika ubora wa hali ya juu.

Rais Dk Mwinyi ameipongeza Tume hiyo kwa kuendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa ustadi mkubwa, ambapo uandikishaji wa wapiga kura ulifanyika kwa utulivu.
Amehimiza wananchi ambao hawajachukua vitambulisho vyao vya kupigia kura kutimiza wajibu wao na kuhakikisha wanatumia haki yao ya kidemokrasia kwa utulivu na kuilinda amani ya nchi.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar umemtunukia Rais Mwinyi tuzo maalum ya kutambua utendaji na juhudi zake za kuimarisha demokrasia nchini pamoja na kukamilika kwa jengo hilo.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Watendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Viongozi wa vyama vya Siasa, Taasisi za Ujenzi, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.


