1,369 wachunguzwa moyo Sabasaba

DAR ES SALAAM; Watu 1,369 wakiwemo watu wazima 1,289 na watoto 80 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya Sabasaba yaliyomalizika Julai 13.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi hiyo, Anna Nkinda amesema baada ya kufanyiwa vipimo vya moyo na kupata matibabu, watu 217 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI ikiwa ni pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa kina zaidi ambapo watu wazima walikuwa 209 na watoto 8.

“Watu 371 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na watu 336 walifanyiwa kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo, vipimo vya maabara vilifanyika kwa watu 763 ambao walichunguzwa matatizo ya figo, ini, kiwango cha mafuta mwilini, pamoja na homa ya ini.

“Watu 145 walipata elimu ya mtu mmoja mmoja ya ushauri wa lishe na kufuata mtindo bora wa maisha kutoka kwa mtaalamu wetu wa lishe ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo,” alisema Anna.

Anna amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yao hasa pale ambapo taasisi hiyo inakuwa ikitoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo katika programU yake ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan Outreach Services.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika banda hilo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujua afya za mioyo yao zikoje.

“Sijawahi kupimwa moyo katika maisha yangu, baada ya kusikia huduma ya upimaji inapatikana katika maonesho ya Sabasaba niliona nami nije kupima, nashukuru sana moyo wangu uko salama. Nimepewa ushauri wa jinsi ya kuutunza ili usipate madhara siku za mbeleni,”alishukuru Amon Mwasote mkazi wa Mkuranga.

Jemima Masanja mkazi wa Morogoro amesema mtoto wake alikuwa na tatizo la kutokukua vizuri na kuchoka haraka anapocheza na wenzake na alimpeleka katika hospitali kadhaa kutibiwa lakini hakupona.

“Baada ya kufanyiwa vipimo amekutwa na tatizo la tundu kwenye moyo. Amepewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”, amesema

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button