Washauriwa kuzingatia usalama wa watoto kwenye vyombo vya usafiri

SHINYANGA: WAZAZI, walezi na wamiliki wa vituo vya kulea watoto mchana mkoani Shinyanga wameshauriwa kuangalia njia nzuri ya ubebwaji wa watoto wadogo katika vyombo vya usafiri ambavyo vimekuwa vikiwasababishia ulemavu na wengine kupoteza maisha kutokana na kubebwa kwao bila kuzingatia usalama wao na barabarani.
Hayo yamesemwa na Ofisa Usalama Barabarani Wilaya ya Shinyanga kutoka Jeshi la Polisi, Prosper Komaa alipokuwa akitoa elimu kwenye kikao cha wamiliki wa vituo vya kulea watoto mchana mkoani Shinyanga.

Komaa amesema wapo wamiliki ambao bado wanatumia magari ambayo siyo rasmi kwa ubebaji watoto na kuogopa kuyapitisha barabara kuu huku vioo vya madirisha vikiwekwa tinted na kupenyeza kwenye vichochoro ili wasibainike na askari wa usalama barabarani.
“Wamiliki ninawaomba mkague magari yanayobeba watoto yawe na rangi rasmi ya njano iliyoteuliwa msisubiri mpaka tanganzo litolewe na serikali au kutokee na maafa pia magari hayo ndani yawe na waangalizi wa jinsia ya kike na kiume,” amesema Komaa.

Komaa amesema wapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaamini waendesha bodaboda na kuwapakiza watoto zaidi ya wanne kwenye pikipiki moja na wengine kukalia tanki la mafuta hiyo ni hatari ambayo itamfanya mafuta hayo yamuathiri kwenye ubongo wake kadri anavyoendelea kukua mtoto.
Ofisa Ustawi kutoka mkoani Shinyanga Lyidia Kwesigapo amesema wamiliki wa vituo wanatakiwa kuzingatia sheria zilizowekwa kabla ya kusajiliwa kuna vitu wanavyoulizwa sanjari na usafiri wa watoto, mazingira ya kuishi wanapojifunzia.

Muuguzi Mkuu kutoka mkoani Shinyanga, Flora Kajumulo aliyehudhuria kikao hicho amesema anao ushuhuda wa watoto kubebwa kwa kurundikana katika gari moja na watoto wengine kupakizwa kwenye dalala za baiskeli zilizopelekea baadhi ya watoto kuliwa visigino vya miguuni na spoku za baiseli hizo.
Mwenyekiti wa umoja wa wamiliki wa vituo vya kulea watoto wadogo mchana Damari Molles amesema wamekuwa wasisitizana kwenye vikao vyao pindi wanavyokuna na kuhakikisha changamoto walizonazo wanaziondoa.



