Tanzania ya 2050

RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itakayoanza kutekelezwa Julai Mosi mwakani.
Samia ni Rais wa pili wa Tanzania kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo akitanguliwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida alisema Desemba 9, mwaka 2023 Rais Samia alizindua mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwenye makundi mbalimbali.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Fredy Msemwa alisema watu zaidi 1,174,000 wametoa maoni ana kwa ana kwenye kaya zao.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema mchakato wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ulishirikisha makundi yote ya jamii kwa kutumia njia zote za analojia na kidijiti.
Profesa Kitila alisema asilimia 81 ya watu 1,132,837 waliojitokeza kutoa maoni yao kwa njia ya simu, tovuti na mitandao ya kijamii ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35.
“Hii inaakisi demokrasia ya nchi yetu ambapo kwa sasa asilimia 76 ya Watanzania wote wapo chini ya miaka 36, kwa kuzingatia maoni hayo dira hii imeandikwa na vijana ambao wataishi nayo kwa muda mrefu zaidi,’’ alisema.
Dira inayotekelezwa sasa ilianza kutumika mwaka 2000 na itafikia ukomo wake Juni 31, mwakani.
Dira 2050 inaongozwa na misingi sita na msingi wake mkuu ni maendeleo ya watu yanayochochewa na uchumi imara, wenye ushindani na kipato cha juu ili kuinua viwango vya maisha ya wananchi na kuondoa umasikini.
Dira 2050 ina shabaha tatu ikiwemo ya kuiwezesha nchi kuwa ya kipato cha kati ngazi ya juu, ya uchumi wa viwanda, ikiwa na pato la taifa la dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja la Dola za Marekani 7,000 kwa mwaka.
Nyingine ni kutokomeza umasikini uliokithiri, kwa makundi yote na Tanzania kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika na miongoni mwa nchi kumi bora duniani.
Dira hiyo inataka ifikapo mwaka 2050 Tanzania iwe nchi ya mfano katika ustahimilivu, ubunifu, ustawi na diplomasia barani Afrika na duniani ikichochewa na rasilimali zake, miundombinu imara na nguvukazi mahiri na yenye motisha.
“Inatarajiwa kuwa nchi yenye kipato cha kati ngazi ya juu, ikiwa na pato la taifa la Dola za Marekani trilioni moja, na wastani wa pato la mtu mmoja la Dola za Marekani 7,000 kwa mwaka. Uchumi wake utakuwa shindani na mseto, unaotegemea viwanda na ukichagizwa na nguvukazi yenye maarifa na ujuzi,” imeeleza dira hiyo.
Dira 2050 inaweka kipaumbele cha ushiriki wa makundi ya wanawake na vijana katika maendeleo kwa kutumia vipaji, uwezo na ari yao katika kufanikisha ukuaji wa kiuchumi na maendeleo jumuishi.
Dira 2025
Mwaka 2000 Tanzania ilizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 iliyolenga kulijenga taifa kuwa nchi ya kipato cha kati.
Maeneo ya kipaumbele yalikuwa ni kilimo cha kisasa, viwanda, miundombinu na teknolojia. Dira 2025 imeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, ukuaji wa uchumi, na utawala huku kukiwa na ongezeko la ushiriki wa wanawake katika siasa na uchumi.
Tangu kuzinduliwa mwaka 2000, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imekuwa nyenzo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
Msingi wa mafanikio haya umejengwa juu ya misingi ya amani, utulivu na umoja wa kitaifa, hali iliyowezesha utekelezaji wa sera, kuvutia uwekezaji na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Katika nyanja za kiuchumi, Tanzania ilidumisha kasi ya ukuaji endelevu, ambapo pato halisi la taifa liliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa mwaka kati ya 2000 na 2024.
Vilevile, kiwango cha umasikini uliokithiri kilipungua kutoka asilimia 36 mwaka 2000 hadi asilimia 26 mwaka 2024.