Samia ataja sekta tisa za kipaumbele

RAIS Samia Suluhu Hassan ametaja sekta tisa za kipaumbele wakati wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alitaja Dodoma jana wakati akiizindua dira hiyo.
Alisema maeneo ya kipaumbele ni yenye uwezo wa kuzalisha ajira kwa wingi, kuongeza mauzo nje, kuchochea ukuaji wa sekta nyingine, kuongeza thamani ya mazao na kukuza mapato ya serikali.
Akizungumza wakati wa kuzindua dira hiyo, Rais Samia alisema sekta za kipaumbele ni kilimo, utalii, viwanda, ujenzi, madini, uchumi wa buluu, michezo na ubunifu huduma za kifedha na sekta ya huduma.
“Pamoja na vigezo hivi, thamani ya kweli ya Dira 2025 itapimwa kwenye uwezo wetu wa kutafsiri kwa vitendo katika mipango, bajeti na maamuzi mbalimbali, kwa hiyo hatuna budi kuzingatia suala la uwajibikaji wa pamoja.
“Nimatumaini yangu kuwa uzinduzi wa Dira 2050 utaamsha ari ya kila mwananchi kwa nafasi yake kuchangia katika kutosheleza kiu ya Tanzania ya kweli yenye maendeleo endelevu,” alisema.
Alisema kwa sasa kuna hali ya kudorora kwa hali ya kujadili masuala ya maendeleo katika jamii hususani vijana ambao ndio tegemeo la nchi katika kujenga kesho iliyo bora.
“Hii siyo sawa hata kidogo katika miaka 25 ijayo lazima turudishe mijadala ya maendeleo katika nchi yetu ijadiliwe na vijana na wajipange katika utekelezaji wake,” alisema.
Yaliyozingatiwa
Rais Samia alisema ili kuendana na mabadiliko ya mfumo na muundo wa uchimi duniani, Tanzania lazima iendeleze sera ya kutofungamana na upande wowote na kujipanga kulinda maslahi ya taifa katika mazingira mapya ya kikanda na kimataifa.
Pia, alisema Tanzania iendelee kujipambanua na kuwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kulinda mazingira na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Rais Samia alisema pia Tanzania lazima iwekeze katika ustawi wa jamii ili kulinda nguvu kazi ya taifa na kuwa makini na mapokeo ya teknolojia za kisasa ili kulinda ajira za Watanzania.
Alisema pia, ni lazima Tanzania ijipange ili iwe sehemu ya kutumia teknolojia, kusababisha na kumiliki mabadiliko ya teknolojia ikiwamo akili unde.
Rais Samia alisema Tanzania imejiwekea lengo la kujenga taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.
“Tanzania tunayotaka katika miaka 25 ijayo tunapozindua Dira 2050 tujielekeze katika vitendo zaidi kuliko maneno. Serikali, sekta binafasi na wanachi tutende zaidi kuliko kusema hii ina maana kwamba mtihani halisi wa dira hii utakuwa kwenye utekelezaji wake,” alisema.
Maelekezo
Aidha, Rais Samia alitoa maelekezo sita na kusisitiza kuwa ili kufikia lengo na shabaha ya Dira 2050 ya kufikia uchumi wa kati wa juu wa Dola za Marekani trilioni moja ipo haja ya kubadili fikra, mitizamo na namna ya kufanya kazi na kupimana.
“Ni wazi kuwa hatutaweza kufikia lengo hili kama tutaendelea kufanya kazi kwa mazoea; lazima tubadilike kifikra, kimtazamo na kimatendo na lazima tupimane kwa matokeo ya kazi,” alisema.
Aidha, Rais Samia aliielekeza Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuandaa kwa haraka nyenzo zitakazotumika kupima matokeo ya utendaji serikalini kwa kuzingatia lango na shabaha za dira hii kabla ya kuanza utekelezaji wake Julai, 2026.
Pia, alizitaka wizara zote kupitia sera zake na kuhakikisha zinashabihiana na maudhui ya dira na kuelekeza kuwa sera ambazo haziendani hazina budi kurekebishwa kwa haraka na kuielekeza Sekretarieti ya Tume ya Mipango kuratibu utaratibu huo.
Rais Samia pia aliiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza mchakato wa kuchambua na kuja na mapendekezo ya maboresho ya kisheria ili kuwezesha utekelezaji kamili wa dira.
Pia, aliielekeza Tume ya Taifa ya Mipango kuimarisha mfumo wa tathmini na ufuatiliaji na kila taasisi kuwa na mfumo wazi wa majukumu, muda wa utekelezaji na njia ya kupima mafanikio kwa kila hatua.
“Utaratibu wa utekelezaji uzingatie mshikamano wa ngazi zote za serikali kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma, sekta binafsi, jamii na wadau wa maendeleo.
“Kila taasisi ya serikali italazimika kuwa na vigezo vya kupima utendaji vinavyoendana na malengo na shabaha za dira, utekelezaji huu lazima uendeshwe kwa uwazi, taarifa za maendeleo ziwe wazi na zipatikane kwa umma ili kujenga uaminifu na kuhimiza ushiriki wa wananchi katika safari ya kujenga Tanzania tunayoitaka,” alisema.
Rais Samia alisema sekta binafsi ndiyo muhimili wa ujenzi wa uchumi, hivyo aliitaka kujipanga katika kutekeleza malengo na shabaha za dira na kusisitiza kuwa serikali itaweka mazingira ya kuinyanyua sekta binafsi ya ndani.
Katika kuimarisha ushirikishwaji wa jamii, aliagiza kuwepo mkakati wa mawasiliano, elimu kwa umma na uhamasishaji kuhusu dira ili watendaji, wananchi na wadau wa maendeleo waelewe nafasi na michango yao kuelekea mwaka 2050.
Rais Samia alisema Dira 2050 imeweka msisitizo wa kipekee katika suala la haki, kulinda maadili na utamaduni wa watanzania, hivyo alitoa wito kwa Mahakama ya Tanzania na taasisi zote zinazohusika katika utoaji haki kutambua nafasi zao katika kufanikisha malengo ya dira na kutimiza wajibu wao bila upendeleo, huba, chuki au uonevu kwa mtu yeyote.
Pia, alitoa rai kwa taasisi za kijamii zikiwemo taasisi za kidini ambazo ni muhimili katika kujenga jamii yenye maadili kusimama kidete katika ujenzi wa Tanzania yenye maadili.
“Kuna wadadisi wanaweza kuuliza kwa nini kama Taifa tumeweka lengo kubwa, jibu letu ni moja tu; kwa ukubwa wa rasilimali, ari na uwezo wa Tanzania hatuna sababu yoyote ya kutoweka lengo kubwa kwa kesho yetu na ustawi wa taifa letu.”
Rais Samia alimtaja Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kuwa msimamizi mkuu wa dira na mipango ya maendeleo.
“Kama mnavyokumbuka, Dk Mpango alisema kwa anavyojisikia angeomba kupumzika. Lakini nilikuwa namwambia hupumziki, usimamizi wa dira na mipango ya maendeleo ni jukumu lake, kwa hiyo atapumzika kiaina lakini yuko kazini,” alisema.