Vituo vya kulea watoto vyatakiwa kusajiliwa

SHINYANGA: VITUO vya kulelea watoto wadogo mchana mkoani Shinyanga vimetakiwa kusajiliwa na kufuata utaratibu uliowekwa ili kuweza kuwalinda watoto kwa mujibu wa sheria ya watoto namba 21 ya mwaka 2009.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi amesema hayo wakati akifungua kikao kilicho husisha wamiliki wa vituo vya kulea watoto mchana katika kuangalia hali ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka 2025.
Lyamongi amesema kwa mujibu wa taaifa kutoka halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga kuna jumla ya vituo 103 kati ya hivyo vilivyosajiliwa ni 51 sawa na asilimia 49 na makao za watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi yapo nane na kati ya hayo yaliyosajiliwa ni sita tu sawa na asilimia 75.

Lyamongi amesema katika kikao hicho watoke na maazimio na mikakati ya kuhakikisha makao ya watoto na vituo vyote vinasajiliwa hadi kufikia mwezi mwezi Septemba mwaka 2025 na kudhibiti vituo vinavyoibuka na kuanza kutoa huduma pasipo kusajiliwa.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga Lyidia Kwesigabo akielezea hali halisi ya utekelezaji wa PJT-MMMAM kuanzia Mwezi Januari hadi Juni ambapo wamefanikiwa kuzindua mpango mkakati wa mkoa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (Mtakuwwa).
Kwesigabo amesema kumekuwepo na mafanikio ya uandikishaji watoto 567 kwenye vituo 13 vya kulea watoto wadogo mchana na kutoa mafunzo ya elimu ya lishe kwa watoa huduma ngazi ya jamii 28.
“Ninawaomba vituo ambavyo havijasajiliwa wafike kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kwani wataalamu kutoka wizarani wameahidi watakuja kwaajili ya kusajili vituo ili kuwapunguzia changamoto ya kusafiri kwenda mkoani Dodoma kufuata kusajiliwa vituo vyao,” amesema Kwesigabo.



