Pengo: Wazazi msizuie ndoto za watoto

ASKOFU Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ametoa mwito kwa wazazi wasiwe kikwazo kwa watoto kutimiza ndoto zao.

Alisema hayo wakati wa misa takatifu ya kutoa sakramenti ya kipaimara kwenye Parokia ya Mtakatifu Maria Salome Kimara, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

“Mtoto akisema mimi nataka kuwa padri au sista, mimi nataka kusomea uinjinia usiharakie kumkataza au kumwambia huko huendi, kufanya hivyo kunaweza kuwa kinyume na Roho Mtakatifu anayezungumza ndani yake huyo mtoto,” alisema Kardinali Pengo.

Aliongeza: “Tunapowaombea hawa wapendwa wetu tuwaombee watambue lipi wanalolifanya wanapopokea sakramenti hii ya kipaimara na tuwe na lengo la kuwasindikiza na kuwaimarisha katika maisha yao.”

Kardinali Pengo alihimiza watoto hao kutambua kwamba wana wajibu wa kutangaza matendo makuu ya Mungu katika wanayokusudia kuyafanya katika maisha yao.

Alisema wakitambua maagizo ya Mungu, wayazingatie kwa ujasiri bila hofu.

“Wengi wenu hapa ni vijana wenye matazamio ya kesho, mna haki ya kuwa na ndoto na mawazo ya maendeleo, Mwenyezi Mungu hakatazi lakini maandiko yanatuambia katika yale unayoyafanya na kuyakusudia kwa kiwango gani yatatangaza matendo makuu ya Mungu,” alisema.

Aliongeza: “Tuwaombeeni kwamba katika lolote lile mnalokusudia kufanya katika maisha yenu neno la kwanza kabisa ni kujiuliza Mungu anasema nini katika mpango huu ukielewa nini Mungu anataka ufanye hilo ulifanye kwa ujasiri wote.”

Alisema kwa kuwa wamempokea Roho Mtakatifu atawapa mwanga na kuwaongoza katika yote wanayofanya madogo na makubwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button