Uchangiaji damu kuzindua maonesho ajira, ujuzi Iringa

IRINGA: HOSPITALI ya Mkoa wa Iringa leo itashuhudia hamasa kubwa ya vijana kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, waendesha bodaboda na bajaji, wakijitokeza kwa wingi kushiriki shughuli ya uchangiaji damu.
Shughuli hiyo itakayoanza saa 8.00 mchana ni sehemu ya kampeni ya kijamii inayozindua wiki ya maonesho ya ujuzi, fani na ajira mkoani hapa.
“Shughuli hii ni sehemu ya maandalizi ya maonesho hayo yanayoandaliwa na shirika la Tourism Innovation Hub (TIHub) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi kupitia mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) unaotekelezwa na shirika la kimataifa la Swisscontact,” alisema Jonathan Ngonyani, Mratibu wa Mafunzo ya Kiufundi kwa Vijana wa Swiss Contact.
Akizungumzia umuhimu wa zoezi hilo, Eric Kisanga, mbunifu kutoka Chuo Kikuu cha Iringa alisema, “Kuchangia damu ni njia ya kuonesha mshikamano wetu na jamii. Vijana tunapaswa kuwa mstari wa mbele kusaidia maisha ya wengine, kwani afya bora ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa zima.”

Kwa upande wake, Hamid Mkwinda, mwakilishi wa taasisi za vijana mkoani Iringa alisema, “Uchangiaji damu si tu tendo la utu, bali pia ni nafasi ya vijana kujifunza kuwajibika kijamii. Hii ni sauti yetu kama vijana kuwa tuko tayari kuchangia kwa vitendo maendeleo ya taifa letu.”
Shughuli hiyo itaendelea na kampeni ya usafi katika maeneo ya zamani ya stendi ya mabasi ya mikoani mjini Iringa kabla ya mdahalo maalum kuhusu fursa za kiuchumi kwa vijana, utakaofanyika Alhamisi Julai 24 katika Chuo Kikuu cha Iringa.
Akifafanua zaidi kuhusu maonesho hayo, Ngonyani, alisema maonesho hayo yanayofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa ni sehemu ya jitihada za kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za ajira, ujuzi wa fani na ujasiriamali.

“Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kijana: Ujuzi Wako, Fani Yako, Chaguo Lako’, ikihimiza vijana kujitambua na kuchukua hatua madhubuti katika kujenga maisha yao,” alisema Ngonyani.
Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Iringa, Atilio Mganwa, alisema, ushiriki wa vijana katika maonesho hayo ni hatua muhimu ya kulikomboa kundi hilo na taifa kwa ujumla kutoka utegemezi wa ajira za serikali.
Amewataka vijana wa ndani na nje ya vyuo kutumia jukwaa hilo kujitangaza na kuonyesha uwezo wao.
Alisema maonesho hayo yanatarajiwa kuwakutanisha vijana zaidi ya 3,000 na taasisi mbalimbali na kutakuwa na mafunzo ya uandishi wa wasifu (CV), maandalizi ya usaili, uandishi wa miradi ya biashara na namna ya kupata mitaji.
Alisema ufunguzi rasmi wa maonesho utafanyika Julai 26 na unatarajiwa kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa pamoja na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania.
“Maonesho yamekusudiwa kuwajengea vijana mwelekeo wa kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la ajira na ujasiriamali kwa kutumia ujuzi walionao—ikiwemo kuelewa mahitaji ya sekta binafsi, taasisi za fedha na taasisi za mafunzo ya ufundi stadi,” alisema.
Naye Katibu wa Umoja wa Madereva Bajaji Manispaa ya Iringa Ally Seleman, alisisitiza kuwa ni fursa ya kipekee kwa vijana kupata maarifa mapya na mitandao ya kibiashara.
Maonesho hayo yatakuwa ya wazi kwa wananchi wote na hayatahusisha kiingilio.



