TBC, TAMISEMI waitisha shindano la insha shule za sekondari

DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Utangazaji Tanzania (TBC), Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu wameandaa shindano la uandishi wa insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 26 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Julai 22, 2025, Mkurugenzi wa Huduma za Televisheni wa TBC, Happiness Ngasala, amesema shindano hilo linalenga kumuenzi Hayati Mwalimu Nyerere kwa kuhamasisha vijana kuelezea kwa maandishi mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa na litahusu wanafunzi wote wa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Ngasala ameongeza kuwa shindano hilo litakuwa na zawadi mbalimbali kwa washindi, ambapo wanafunzi watano wa kwanza watapewa kompyuta mpakato pamoja na fedha taslimu. Mada kuu za insha zitahusu masuala ya kupambana na ujinga, maradhi na umasikini mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliyapigia kelele kwa nguvu kubwa wakati wa uongozi wake.

SOMA ZAIDI: Washindi Shindano la Uongozi wa Vijana 2023 wapewa tuzo za ALF Accra

“Tunataka wanafunzi waandike insha zitakazoonyesha uelewa wao kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere, huku wakitumia lugha ya Kiswahili pamoja kingereza. Lengo letu ni kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kuelewa historia ya taifa lao,” amesema Ngasala.

Aidha, amesisitiza kuwa kutakuwa na uchunguzi maalum ili kubaini matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) katika uandishi wa insha hizo, na kwamba mshiriki yeyote atakayebainika kutumia mbinu hizo za udanganyifu ataondolewa mara moja kwenye shindano.

Shindano hilo linaanza rasmi leo, Julai 22, 2025, na litahitimishwa Oktoba 14, 2025, siku ambayo taifa huadhimisha kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere. Pia, kilele cha shindano hilo kitaambatana na mbio za pole zijulikanazo kama “Mwalimu Nyerere Marathon.”

Wanafunzi wote wa sekondari nchini wanahimizwa kushiriki kwa wingi katika shindano hilo ili kuenzi urithi wa Baba wa Taifa kwa njia ya maandishi. Utaratibu rasmi wa kushiriki utatangazwa hivi karibuni kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ya TBC na Wizara husika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button