Bandari kavu Kwala, mizigo SGR vyanoga

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Bandari kavu ya Kwala na safari za ubebaji wa mizigo kwa kutumia treni ya mwendokasi ya SGR kwenda Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alisema pia Rais Samia atazindua kituo cha matengenezo ya vichwa vya treni na uwanja wa kupanga mabehewa ya treni kwenye eneo hilo la Kwala katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Kunenge alisema Rais Samia atafanya kazi hizo Julai 31, mwaka huu.

Aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake Kibaha kuwa Bandari kavu ya Kwala ni ya kisasa na itakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 823 kwa siku na makasha 300,000 kwa mwaka.

Kunenge alisema bandari hiyo imejengwa kuongeza tija na kuondoa msongamano wa makasha kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 30.

“Pia, kuondoa msongamano wa magari makubwa yanayosafirisha mizigo kwenda mikoani na nje ya nchi na Rais ametoa maeneo kwa nchi zinazounganishwa na barabara,” alisema.

Alizitaja nchi hizo kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi, Zimbabwe, Uganda na Sudan Kusini.

Alisema Somalia na Sudan wameonesha nia kupata maeneo katika Bandari kavu ya Kwala.

“Pia, atapokea mabehewa 160 ya reli ya kati ambapo 20 yamekarabatiwa na setikali imenunua mapya 100 huku mengine yakiwa yamekarabatiwa na shirika la chakula duniani, mengine wakala wa uwezeshaji ushoroba wa kati,” alisema Kunenge.

Alisema pia, Rais ataweka jiwe la msingi kwenye kongani ya viwanda iliyopo Kwala ambako kutajengwa viwanda 250.

Kunenge alisema viwanda saba vimeanza kazi na vitano viko kwenye hatua za ujenzi.

“Huduma zote zipo barabara, maji na inafikika kwa urahisi, hivyo viwanda vitaongezeka kwa wingi na kutakuwa na ugeni mkubwa wa viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Mabalozi na wadau mbalimbali,” alisema.

Kunenge alisema baada ya kufanya matukio yote hayo Rais atafanya mkutano kwa kuongea na wananchi wa Mkoa wa Pwani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button