Dk Nagu aridhishwa ukusanyaji mapato hospitali Handeni Mji

TANGA: Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia afya, Profesa Tumaini Nagu, ameipongeza Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni kwa ukusanyaji mzuri wa mapato na usimamizi wa miradi ya afya na hivyo kusaidia kutoa huduma nzuri kwa wananchi.
Ametoa pongezi hizo jana alipotembelea hospitali hiyo na kupokea taarifa ya utekelezaji wa Idara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kutoka kwa Mganga Mkuu, Dk Hudi Shehdadi.

Amesema kuwa ni dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuona wananchi wake wanapata huduma hivyo usimamizi mzuri wa mapato unasaidia hospitali kutoa huduma bora
Hata hivyo Prof. Nagu ameahidi kuwa Serikali kupitia TAMISEMI itaendelea kuboresha huduma za afya ikiwemo kutatua Changamoto zilizopo katika Halmashauri ya Mji Handeni.

Awali akitoa taarifa Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dk Hudi Shehdadi amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Idara ya Afya ilipanga kukusanya Sh bilioni 1.67, lakini hadi Juni 2025 imekusanya Sh bilioni 1.76 bilioni, sawa na asilimia 105 ya lengo.
Aidha, amesema mapato hayo yamesaidia uendelezaji wa miundombinu kwa kiasi cha Sh milioni 133.02, huku mfuko wa jimbo ukitoa Sh milioni 29.4 kwa ukamilishaji wa zahanati tatu.




