Pemba yaomba mafunzo ya dharura udaktari

PEMBA : TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeombwa kuwajengea uwezo madaktari kisiwani Pemba, Zanzibar ili waweze kutoa huduma za msingi kwa majeruhi wa ajali zinazohusisha mifupa na ubongo.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdulla Said, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya elimu ya juu yanayoendelea katika viwanja vya Gombani, Pemba.

Said amesema visiwa vya Pemba vinakabiliwa na changamoto ya ajali za barabarani, lakini huduma za awali kwa majeruhi zinakosekana kutokana na upungufu wa ujuzi wa madaktari wa eneo hilo.

“Mnajua changamoto ya usafiri iliyopo hapa Pemba. Bodaboda akipata ajali, inakuwa vigumu kumpatia huduma ya msingi ya mifupa na ubongo. Tunaomba muwajengee uwezo madaktari wetu ili wagonjwa wapate huduma bora kabla ya kupelekwa hospitali kubwa,” alisema Said.

Aidha, alitoa pongezi kwa MOI kwa kushiriki maonesho hayo kwa mara ya kwanza kisiwani humo, akisema taasisi hiyo kama kituo cha umahiri inapaswa kuendeleza mpango wa kusaidia wataalamu wa Pemba.

Kwa upande wake, Dk Catherine Hance kutoka MOI amesema lengo la kushiriki kwenye maonesho hayo ni kutoa elimu na huduma ya ushauri kwa wananchi. SOMA: Wataalamu wa ganzi, usingizi kujifunza njia za kisasa MOI

“MOI tunatoa huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, mgongo na mishipa ya fahamu. Kupitia programu ya ‘Tiba Mkoba’, tunawajengea uwezo wataalamu wa maeneo husika ili waweze kutoa huduma hizo karibu na wananchi,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button