NEDC yatafsiri Dira 2050 maendeleo kwa vijana

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete amesema Chama cha kitaifa cha Biashara na Maendeleo (NEDC) kimefanikiwa kutafsiri Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuhusu malengo ya kuwawezesha vijana.
Ridhiwani aliyaeleza hayo jana Dar es Salaam, alipozindua rasmi chama hicho chenye lengo la kuunganisha nguvu kati ya sekta binafsi, serikali, taasisi za kifedha na vijana wa Kitanzania wanaotafuta maendeleo kupitia ubunifu, ujasiriamali na biashara endelevu.
“Kwa ndoto mliyonayo NEDC, mmefaikiwa kutafsiri Dira 2050 ambayo kwa kweli inaeleza kinagaubaga ni jinsi gani tunaweza kufikia malengo ya kuwasaidia vijana wa Kitanzania,” alieleza Ridhiwani.

Alisema vijana wanayo mawazo ambayo yanaweza kuwa ya kujenga lakini changamoto kubwa imekuwa kutokuwa na elimu ya jinsi ya kujiandaa kuwasilisha mawazo yao kwa namna nzuri yenye kushawishi wawekezaji kuwekeza katika mawazo hayo.
“Kikubwa siyo kuwa na ubunifu hapana, inachukua zaidi ya ubunifu ili kufikia malengo yako kwa sababu leo hii mimi naweza kuwa nipo lakini tamaa yangu mimi ni kumiliki mfano hoteli, je kwa sababu jina langu Kikwete ndio inaweza kuwa sifa mimi kukopesheka haiwezi kuwa hivyo, lazima uwe na uwezo wa kujiwekea mazingira ya mtu kuwekeza katika ubunifu wako,” alieleza.
Pia, aliziomba taasisi za kifedha kama benki ya CRDB ambayo imekuwa ikijihusisha katika kusaidia kuinua biashara changa kutengeneza mazingira ya vijana kuwa na nidhamu ya kifedha ili kufikia malengo yao.

“Unachokiona leo hii kwa waliofanikiwa kama akina Bill Gates, walianza biashara zao ndogo wakiwa kwenye mazingira ya chini lakini akaja mtu mtu mmoja tu akasema mimi naamini katika wewe, akaweka pesa baada ya hapo wakajenga uwezo na kwa sababu walikuwa na nia na nidhamu ya kufikia malengo kwamba wanaweza wakakopesheka leo hii ni wakubwa kuliko unavyoweza kueleza,” alifafanua.
Aliongeza kuwa “Sisi kama serikali tutaendelea kuwasaidia pia ni mkakati wa serikali na kisera ambao umeainishwa ndani ya Ilani ya CCM ya miaka mitano inayokuja kwamba serikali itakazana kuhakikisha inawasiaida vijana kuweza kupata mikopo mbalimbali na fursa zilizopo ambazo zinatokana na fedha za ndani na za nje pia.”
Kwa upande wake Mwanzilishi na Mwenyekiti wa NEDC, Jesse Madauda alisema dhamira yao ni kuwezesha, kukuza na kuwalinda wabunifu na wajasiriamali wa Tanzania hasa vijana na wanawake kupitia mifumo rasmi ya mendeleo, mafunzo, fursa za masoko na upatikanaji wa mitaji.
Alisema maono yao yanalingana kikamilifu na Dira ya taifa ya maendeleo ya 2050 ambayo inatamka bayana kuwa 2050 Tanzania itakuwa na uchumi wa kati wa juu unaotegemea ubunifu, teknolojia na usawa wa kijamii.
“Moja ya programu mahiri ya NEDC ni Bongo Fursa, mpango maalum wa kugundua, kulea na kuinua vipaji vya ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa vijana wa Kitanzania,” alieleza.



