Wananchi Kwedizinga kunufaika mradi wa maji wa mil 297/-

TANGA: Zaidi ya wananchi 4,486 waliopo kijiji cha Kwedizinga wilayani Handeni watanufaika na huduma ya maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa zaidi ya Sh milioni 297.
Uzinduzi huo umezinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian ambapo amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika na taasisi binafsi katika kuleta maendeleo.

DC Nyamwese ameeleza kuwa mradi huo ni matokeo ya ushirikiano wa dhati kati ya Benki ya ABSA Tanzania na Shirika la World Vision Tanzania na hivyo kusaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa maji kwenye eneo hilo.

“Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi thabiti wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote wa maendeleo kwa lengo la kuimarisha huduma za kijamii na kupunguza changamoto za wananchi”amesema Mkuu wa Wilaya huyo.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Vision Tanzania, James Anditi amesema kuwa mradi huo unatokana na simulizi yamtoto Shania aliyoitoa kwenye mkutano wa dunia wa mazingira (COP27) uliofanyika nchini Misri.



