Msambatavangu na ndoto ya Iringa Mjini kuwa Geneva

IRINGA: Mbunge wa Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Jesca Msambatavangu, amerejea tena uwanjani kwa kishindo baada ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kurudisha jina lake katika safari ya kuwania muhula mwingine wa ubunge.
Akizungumza baada ya uteuzi huo, Jesca alionekana mwenye ari, akisisitiza dhamira yake ya kuendeleza safari ya maendeleo kwa kushirikiana na wananchi waliompa dhamana hiyo tangu 2020.
Katika ujumbe wake kwa wana CCM na wananchi wa Iringa Mjini, Jesca hakusita kuweka wazi malengo makubwa yanayomchoma moyo – kulifanya jiji la Iringa kuwa Geneva ya Tanzania. Kauli hii si tu yenye mvuto bali ni alama ya maono mapya kwa mji unaoendelea kuimarika kiuchumi, kielimu, kiafya na kijamii.
“Nimerudi kwa sababu kazi bado haijaisha. Tuna mengi tuliyoanza, na mengi zaidi tunayotakiwa kuyakamilisha kwa pamoja,” amesema Jesca kwa kujiamini.
Katika kipindi chake cha miaka mitano, Jesca ametajwa kuwa miongoni mwa wabunge waliotekeleza kwa vitendo. Mchango wake katika sekta ya afya umesababisha kujengwa kwa zahanati nne mpya, ukarabati wa vituo vya afya na Hospitali ya Frelimo.
Upande wa elimu, takwimu zinasema yote – madarasa 130 yamejengwa, shule mpya tisa zimefunguliwa, na walimu 410 wameajiriwa.
Na mambo hayakuishia hapo. Jesca ameongoza jitihada za kupanua huduma za maji safi hadi kufikia asilimia 97 ya wananchi, huku pia mitaa mingi ikiunganishwa na huduma ya umeme.
Katika sekta ya haki za watoto na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, amekuwa sauti ya walionyamaza, akihakikisha wahalifu wanachukuliwa hatua.
“Nataka Iringa Mjini iwe kitovu cha ubunifu, biashara na huduma bora. Nataka watoto wetu wasome kwenye madarasa bora, mama zetu wajifungue salama, na vijana wapate fursa za ajira na mitaji,” amesema.
Kwa upande wa wafanyabiashara wadogo, Jesca ameahidi kwamba awamu inayokuja itakuwa ni ya kumalizia changamoto zao kikamilifu kwa kushirikiana na mamlaka husika.
Kwa muktadha wa maendeleo ya Iringa Mjini, Jesca haonekani kama mgombea wa kawaida – bali ni kiongozi mwenye historia ya utekelezaji, mwenye dira, na mwenye maono yanayoeleweka.
Kama kuna wakati wa Iringa kuimarika zaidi, basi ni sasa – na kama kuna mtu wa kuipeleka huko, basi ni Jesca Msambatavangu, amesema mwenyewe.



