Ouattara kutafuta muhula wa nne Ivory Coast

ABIDJAN, IVORY COAST : RAIS wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, ametangaza rasmi nia ya kuwania tena urais kwa muhula wa nne katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Tangazo hilo limeibua mvutano wa kisiasa nchini humo, hasa kutokana na historia ya kubadilishwa kwa katiba mwaka 2016 ambayo iliondoa ukomo wa mihula ya urais.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 83 amesema anaruhusiwa na katiba mpya kuwania tena, licha ya awali kuahidi kuwa hangewania muhula mwingine. SOMA: Rais Ivory Coast kugombea tena.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Ouattara alishinda muhula wa tatu baada ya kifo cha aliyekuwa mrithi wake aliyeteuliwa, Waziri Mkuu Amadou Gon Coulibaly, hali iliyomlazimu kurejea ulingoni.
Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa na baadhi ya wapinzani wake, wakiwemo waliowekwa kando na sheria za uraia pacha. Mpinzani wake mkuu, Tidjane Thiam, tayari amepigwa marufuku na mahakama kuwania urais kwa tuhuma za kuwa na uraia wa Ufaransa alipotangaza nia yake, ingawa ameshaukana uraia huo.



