KIMAS, serikali wajadili mipango maendeleo ya watoto

MTWARA: TAASISI isiyo ya kiserikali ya Kitovu cha Maendeleo Safi (KIMAS) mkoani Mtwara imekutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwemo wa serikali na binafsi wanaotekeleza afua mbalimbali za watoto ili kutengeneza mpango kazi juu ya namna bora ya kutekeleza na kuchagiza programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto.
Akizungumza wakati wa kikao kilichokutanisha wadau hao kutoka sekta hizo mbili, Mtendaji Mkuu wa KIMAS Torai Kibiti amesema programu hiyo inahusisha watoto wenye umri kuanzia mwaka 0 hadi miaka 8 kilichofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Aidha, lengo la kikao hicho ni kufanya tathimini ya utendaji kazi uliofanyika kwa kipindi kilichopita na kutaja baadhi ya wadau wanaotekeleza program hiyo ikiwemo vituo vya kulea watoto wadogo mchana (Day Care).

Pia mashirika madogo yasio ya kiserikali pamoja na viongozi wa serikali ambao ni maofisa lishe pamoja na maofisa ustawi wa jamii.
“Kwa siku ya leo tumewaita wadau kutoka katika sekta binafsi na za serikali kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa kazi uliofanyika katika kipindi kilichopita na kuandaa mpango kazi juu ya kuchagiza katika program hii jumuishi ya malezi makuzi na maendeleo ya awali kwa watoto,” amesema Torai.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mtwara, Theresia Ngonyani amesema wanaendelea kutoa elimu katika jamii kuhusu program hiyo ili kuondoa mmomonyoko wa maadili unaotokana na kutozingatia makuzi na malezi kwa watoto.
Pia kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza kwa mtoto kuanzia umri wa mwaka 0 hadi miaka 8 ili kupunguza kuwa na watoto wasio kuwa timilifu.

“Ubongo wa mtoto huingiza vitu vingi kuanzia umri wa mwaka 0 hadi miaka 8 hivyo program hii tumeipeleka hadi kwa ngazi za kata na vijiji, tunaamini tukiwekeza katika umri huu tutapunguza vitendo vya mmomonyoko wa maadili pamoja na uwepo wa watoto wasio timilifu,”amesisitiza Theresia
Hata hivyo ameeleza kuwa kuna vipengele ambavyo hujumuisha program hiyo ya malezi ,makuzi,na maendeleo ya awali ya watoto ikiwa ni pamoja na lishe iliyo bora ,afya, fursa ya ujifunzaji wa awali, ulinzi na usalama wa mtoto na malezi yenye muitikio.



